Watu wanane  wamefariki dunia papo hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa vibaya, akiwemo Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Mbeya Mh. Mary Mwanjelwa,  baada ya lori la mafuta lenye nambari za usajili T81 4BTC na tela lenye namba T815 BTC lililokuwa likitelemka katika mlima wa Lwambi Mji wa Mbalizi kufeli breki na kwenda kuyagonga magari matatu ambapo kati ya hayo magari mawili yaliteketea kwa moto. 

 Ripota wa habari hii kutoka jijini Mbeya anaendelea kutupasha kuwa ndani ya gari la Mbunge huyo kulikuwepo na watu wawili ambapo dereva wa gari hilo alijeruhiwa miguuni na kichwani huku mwanamke mmoja anayesadikiwa kuwa Katibu wa Mbunge huyo ambaye jina lake halikufahamika mara moja inadaiwa kuwa ameteketea kwa moto. 

Akizungumza na waandishi kwenye eneo la tukio,Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Mhe. Abbasi Kandoro alisema ajali hiyo imetokea kwa magari manne ambapo kati yao matatu yameteketea kwa moto papo hapo likiwemo gari la Mbunge Toyota Hilux. Alisema, gari lingine lililoteketea kwa moto ni gari ndogo ya abiria aina ya Toyota Hiace yenye namba T587 AHT ambalo lilikuwa na watu kumi ambao kati yao wapo waliofariki na kujeruhiwa na lori lenyewe la mafuta limeteketea kwa moto. 

Akizungumzia tukio hilo kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya, Afande Diwani Athumani alisema baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo ni Mbunge Mary Mwanjelwa ambaye anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Teule ya Ifisi baada ya kuumia kwenye kiuno na dereva wake ambaye ameumia miguu na kupata majeraha kichwani. 

KAmanda amesema majeruhi wengine wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali Teule ya Ifisi na wengine hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na kwamba hali ya Mbunge inaendelea vizuri. Ripota wa habari hizi alizungumza na baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo ambao walisema kuwa Lori hilo la mafuta lilikuwa likishusha mlima huo wa Lwambi, huku mbele yake kukiwa na Lori lingine la mizigo ambapo dereva wa gari hiyo alifanikiwa kulipisha Lori hilo na ndipo lilipoyagonga magari hayo mawili ambayo mbali na kupinduka kandokando ya barabara pia yaliteketea kwa moto. 

“Lori la mafuta lilikuwa katika mwendokasi na ndipo lilipoligonga lori lingine la mizigo na kisha kwenda kuyagonga magari madogo mawili na kusababisha ajali hiyo kutokea,”alisema shuhuda Alisi Mwakisapi. 
Alisema, Mbunge wa viti maalumu Mhe Mary Mwanjelwa aliokolewa na bodaboda iliyokuwa karibu na eneo hilo kwa kile alichokidai kuwa mara baada ya kufanikiwa kutoka ndani ya gari hilo dereva huyo alimuona na kumchukua kwenye bodaboda na kumuwahisha hospitali.

 “Katika gari alilokuwa amepanda Mbunge, alikuwemo dereva na mwanamke mmoja ambaye anadaiwa kuteketea kwa moto,”alisema 


Miili ya marehemu tisa imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Mbeya na hospitali Teule ya Ifisi majina yao hayajatambuliwa na kwamba mwili wa mwanamke mmoja ambaye alikuwa kwenye gari ya Mbunge uliteketea kwa moto. 

Baadhi ya maiti zikiwa zimehifadhiwa sehemu moja kabla ya kupelekwa hospitali.
Mkuu wa mkoa Mbeya,Abas Kandoro akiangalia ajali iliyotokea mbalizi mbeya mchana wa leo


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. pole wafiwa.Inabidi serikali iwe unayafanyia inspection hayo malori na mabasi kila baada ya miezi mitatu.Huku Marekani huwa tunafanyiwa inspection kila siku 90.

    ReplyDelete
  2. anko, ukimuona mkuu wa zimamoto na uokozi mwambie vijana wanaulizia zile fedha tunazokatwa kwa lazima kila mwaka kwa ajili ya faya tingisha na ukaguzi wa gari zimetumika wapi?

    ReplyDelete
  3. naanza kuamini kuwa laana ya binadamu inatoka/ inaletwa na binadamu wenyewe. kabla ya serikali kuanza kulazimisha malipo ya fire hatukuwa na matokeo ya moto mengi na mabaya kama sasa. tumejilaani wenyewe kwa tamaa ya kunyang'anya kila kitu kwa kigezo cha kuchangia.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...