Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mh . Hawa Ghasia (kulia) akiteta jambo na mtaalamu wa masuala ya biashara kutoka Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) Wille Magehema katika mkutano maalumu wa ushirikiano kwa manufaa ya wote (smart partnership dialogue) uliohusisha wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa mikoa.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia (kulia) akibadilishana mawazo na mtaalamu wa masuala ya biashara kutoka Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) Wille Magehema katika mkutano maalumu wa ushirikiano kwa manufaa ya wote (smart partnership dialogue) uliohusisha wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa mikoa.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Bishara la Taifa (TNBC), Bw. Samson Chemponda (kulia) akimsikiliza kwa makini Inspekta Jeneral wa Polisi (IGP), Said Mwema muda mfupi mara baada ya kumalizika kwa mkutano maalumu wa ushirikiano kwa manufaa ya wote (Smart Partnership Dialogue) uliohusisha wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa mikoa, katikati ni mtaalamu wa masuala ya biashara kutoka baraza la biasha la Taifa (TNBC), Mr. Wille Magehema.

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda, amewataka viongozi wa serikali nchini kuchukulia kwa umakini suala la Ushirikiano wa manufaa kwa wote (smartpartership dialogue) kuwa moja ya chachu kubwa ya kuleta maendeleo katika maeneo yao na Taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki mjini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mkutano maalumu wa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa mikoa juu ya ushiriki wao katika majadiliano ya pamoja ya kuhusu ushirikiano kwa manufaa ya wote.

“Mikutano ya ‘smart partnership Dialogue’, ni tofauti na mikutano mingine, hili ni jukwaa la majadiliano kati ya serikali na jumuiya mbalimbali za wananchi kuhusu jambo lolote lenye manuafaa kwao, na ambalo kwa namna moja ama nyingine litaleta maendeleo yao kijamii na kiuchumi,” alisisitiza Mh. Pinda.

Alisema Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa ujulikanao kama “ Global 2013 Smart partnership Dialogue” na hii ni kutokana na ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa wakati alipohudhuria mkutano kama huo Petrojaya nchini Malaysia mwezi Juni mwaka 2011, mkutano ulioitwa “ Langkawi smart partnership dialogue”.

Aliongeza kuwa lengo la majadiliano haya ni kupata maoni na mawazo kutoka kwa watu wa kawaida kuanzia ngazi za chini mpaka juu, dhana hii inatambua kwamba kila mtu anao mchango wake kwenye jumuiya anayoishi ili kuleta mabadiliko katika jamii.

“Katika hili ndugu zangu, viongozi wa ngazi za juu serikalini hukaa pamoja kama watu wa ngazi sawa na jumuiya za wananchi, zikiwemo za vijana, wasomi, wafanyakazi, wafanyabiashara, waandishi wa habari, wanasanaa, wanasiasa, madhehebu ya dini na kwa ujumla wake jumuiya hizi hujulikana kama smart partnership links” alisisitiza Waziri Mkuu.

Alisema serikali kwa sasa ina mkakati mzuri wa kutambua mchango wa wabunifu na wagunduzi katika kuendeleza sayansi na teknolojia, huku akisisitiza kuwa jukwaa hili la kimataifa liwe sehemu kupanua ushirikiano wa kimataifa katika nyanja ya teknolojia na ubunifu.

“Kuna wagunduzi wanaopatikana kule, hivyo ni lazima kuwe na mikakati ya kuwabaini na kuwaendeleza ili kazi zao zaisaidie kuendeleza uchumi wa nchi yetu na kujiletea maendeleo miongoni mwetu” aliongeza Waziri Mkuu.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) Bw. Samson Chemponda, alisema majadiliano hayo yanatoa fursa hasa kwa mabaraza ya biashara ya mikoa na wilaya katika kuweka mikakati yao ya kibiashara katika maeneo yao hasa kwa kushirikisha wadau wa eneo husika katika ushiriki wao.

“Sisi tukiwa ni wahusika wakuu katika hili tutahakikisha kuwa mpango huu unafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika nchi hii, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha kuwa wananchi katika kada zote wanatambua na kuelewa dhana hii kwa ukubwa na upana wake,” alisema Chemponda.

Alisisitiza kuwa wao kama baraza wanalojukumu kuhakikisha kuwa ushirikiano wa manufaa kwa wote unaeleweka kwa kutoa elimu kwa wadau wote ili kuleta manufaa kwa jamii nzima.

Elimu ndo msingi wa kila kitu, tutahakikisha tunatoa elimu kuhusu dhana hii katika ngazi zote za uongozi na sehemu mbali mbali hapa nchini ili kila mtu aweze kushiriki katika nafasi yake kama mwananchi na kutoa mawazo yake,” alisisitiza Bw. Chemponda.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...