Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa
leo, Alhamisi, Februari 7, 2013, ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Mkuu Dkt. Alex Malasusa
kuombeleza kifo cha Askofu Thomas O. Laizer wa Jimbo la Kaskazini Kati Arusha la
KKKT aliyeaga dunia jioni ya leo.
Katika
salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Askofu Mkuu Malasusa: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na
huzuni nyingi taarifa za kifo cha Askofu Thomas Laizer ambaye nimejulishwa kuwa
ameaga dunia muda mfupi uliopita, jioni ya leo, katika Hospitali ya Rufaa ya
Selian, Arusha.”
“Askofu
Thomas Laizer ametutoka lakini tutaendelea kumkumbuka kama kiongozi aliyetoa
mchango mkubwa katika uongozi wa kiroho wa Watanzania na ambaye wakati huo
alitafuta namna bora zaidi ya kuwatumikia waumini wake. Daima atakumbukwa kama
kiongozi ambaye alitumia vipaji vyake vyote kuwatumikia waumini wake na wote
waliokuwa chini yake.”
Ameongeza
Rais kikwete: “Kufuatia msiba huu mkubwa, nakutumia wewe Baba Askofu Mkuu Alex
Malasusa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kukupa pole ya msiba huu
na kupitia kwako kuwapa pole nyingi maaskofu na viongozi wenzako katika KKKT
pamoja na waumini wote wa Kanisa kwa kuondokewa na kiongozi mwenzao na muumini
mwenzao.”
Aidha,
Rais Kikwete ameongeza, “Pia kupitia kwako Baba Askofu Mkuu, natuma
salamu nyingi za moyoni mwangu kwa familia na wana-ndugu wa Marehemu Thomas
Laizer. Naungana nao katika kuomboleza.
Naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na Baba, Babu na
mhimili wa familia. Nawaombea subira ili waweze kuvuka kipindi hiki kwa sababu
yote ni Mapenzi ya Mungu. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu,
Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Thomas Laizer. Amen.”
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
07
Februari, 2013
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...