Balozi Ignace Gata Mavita wa Lufuta, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika Umoja wa Mataifa, akilizugumza Baraza Kuu la Usalama la UM, mara baada ya Katibu Mkuu, Ban Ki Moon kuwasilisha mbele ya Baraza hiyo Taarifa yake kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Maziwa Makuu. Katika maelezo yake, Ban Ki Moon amelitaka Baraza kuridhia  haraka iwezekanavyo upelekaji wa Brigedi Maalum (intervention Brigade) katika  DRC.  Brigedi hiyo   itakuwa na dhamana pana ikiwamo ya  kukabiliana na  makundi ya  wanamgambo wenye silaha ndani ya DRC na wanaotoka nje ya nchi hiyo na hususani katika eneo la Mashariki ya nchi hiyo.



Na Mwandishi Maalum

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amelitaka Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha haraka iwezekanavyo upelekaji wa   Brigedi  maalum ya  Kijeshi  katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC) ili  iweze kukabiliana na tishio la usalama na amani katika eneo hilo.
Mkuu huyo wa UM ametoa wito huo siku ya jumanne, wakati alipowasilisha mbele ya Baraza hilo , taarifa yake kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na eneo la Maziwa Makuu.
Akilizungumza  Baraza hilo, Katibu  Mkuu ameeleza bayana kwamba hali katika    DRC ni tete na inahitaji maamuzi ya haraka.
Brigedi hiyo  maalum ijulikanayo kama  Intervention Brigade itakuwa na uwezo wa  kutekeleza majukumu yake kwa, ama  kushirikiana au kutoshirikiana na  Jeshi la kitaifa la DRC, dhidi ya  makundi mbalimbali ya wanamgambo wenye silaha   ambao wamekuwa wakihatarisha hali ya amani na usalama  katika eneo la Mashariki ya  DRC.
Katika  taarifa yake kwa  Baraza la Usalama la UM, Ban Ki Moon amependekeza kwamba   Brigedi hiyo maalum itakuwa chini ya  Misheni ya Kutuliza  Amani ya Umoja wa Mataifa katika DRC maarufu kama  MONUSCO kwa mwaka mmoja
“ Brigedi hii maalum na ambayo chimbuko lake  linatokana na  maamuzi ya  Kikanda  inalenga katika kukabiliana na  tishio dhidi ya hali ya utulivu na usalama na itawajibika katika kujibu mapigo    kupitia MONUSCO.
Katibu Mkuu  amebainisha zaidi kwa kulieleza Baraza Kuu la Usalama kwamba, Brigedi hiyo ( Intervention Brigade) itakuwa na dhamana ya  kukabiliana  dhidi ya  kupanuka kwa makundi yenye silaha ya  Kikongo na yale ya kigeni, kupunguza nguvu za makundi hayo pamoja na kupokonya silaha. Na kwamba  upelekwaji wa  Brigedi  hicho utaongeza nguvu.
Kuanzishwa kwa  Brigedi hiyo maalum kunalenga kuunga mkono Mpango mpya wa amani, ulinzi na ushirikiano kuhusu DRC na eneo la maziwa Makuu, mpango ambao ulitiwa saini na viongozi kadhaa wa Afrika   Februari 24, 2013 Addis Ababa, Ethiopia.
Aidha katika upelekaji wa Brigedi hiyo maalum  Umoja wa Mataifa   utakuwa  mdhamini  ukishirikiana  na Umoja  wa  Arika,  Jumuiya ya Mendeleo ya Nchi za Kusini  mwa Afrika ( SADC) na Mkutano  wa Kimataifa wa  Nchi za Maziwa Makuu ( ICGLR).
Baada ya kuwasilisha taarifa  yake, akitekeleza agizo la  Baraza  Kuu lililomtaka kuwasilisha taarifa kuhusu hali ya DRC na hatua ambazo anachukuwa. Hatua inayofuata ni kwa Mkuu huyo wa UM kumteua  Mwakilishi wake Maalum, ambaye kwa kushirikiana na wadau wengine, anatarajiwa kuunga mkono  utekelezaji wa makubaliano yaliofikiwa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...