Na Mwandishi wetu,Arusha
Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini vinatarajia kuhudhuria kongamano la tano la vyuo vikuu linaloanza leo jijini Arusha.
Kongamano hilo la siku mbili limetayarishwa na Kamati ya Makamu wakuu wav you vikuu nchini na wakuu wa taasisi za elimu Tanzania (CVCPT) kwa ushirikiano na wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na wadau wengine wa maendeleo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chuo Kikuu Mzumbe ambacho ndio mwenyekiti wa CVCPT kwa sasa, mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo anatarajia kuwa waziri wa elimu na mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa.
Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu ni jinsi gani vyuo vikuu vinaweza kushirikiana na wadau wengine kama viwanda na makampuni ili kujenga elimu ya juu endelevu Tanzania.
“Mtazamo wa mwaka huu ni jinsi gani taasisi za elimu ya juu zinavyoweza kushirikiana na wadau wengine kama kampuni na viwanda na kuangalia jinsi gani ushirikiano huu unaweza kuimarishwa,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mada hiyo imechaguliwa mahsusi kwa kuzingatia changamoto zinazokabili vyuo vikuu kwasasa hasa jinsi ya kushirikiana na taasisi nyingine kutayarisha wahitimu ambao wako tayari kufanya kazi kwa ufanisi baada ya kuhitimu vyuo vikuu.
Kongamano hilo litawakutanisha wadau wa vyuo vikuu pamoja na wawakilishi wa sekta mbalimbali kwa nia ya kuimarisha mitaala ya vyuo hivyo ili kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa yanayotakiwa kwenye soko la ajira.
Kongamano hilo linataka kukumbusha vyuo kuwa vina wajibu mkubwa katika swala zima la utafiti na ubunifu ili kufikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuongeza ushirikiano na sekta mbalimbali.
CVCPT ilianzishwa mwaka 2005.
Wajumbe wa CVCPT ni makamu wakuu wa vyuo vikuu pamoja na wakuu wa taasisi za elimu binafsi na vya umma pamoja na katibu mtendaji wa TCU.
Kama mwenyekiti wa sasa wa CVCPT, Chuo kikuu Mzumbe kimekua kikitayarisha kongamano hilo kwa mwaka wa pili mfululizo sasa.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...