*Yachangia dola za marekani 155,000 kwa shule aliyosoma Waziri Mkuu



KAMPUNI ya Huawei ya China  ina mpango wa kuzisaidia shule za sekondari 150 nchini Tanzania ili ziwe zikipata mafunzo kwa njia ya mtandao wa mawasiliano (E-Education) kama njia ya kukabiliana na uhaba wa walimu na vitabu vya masomo.



Hayo yameelezwa jana (Jumapili, Oktoba 20, 2013) na Rais wa Kampuni hiyo, Bw. William Xu alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenye makao makuu yao jijini Shenzhen, China.



Alisema walipokea maombi ya Serikali ili kuona jinsi mkongo wa mawasiliano ya Taifa (NCITBB) utakavyoweza kuinua kiwango cha elimu ya watoto wa Kitanzania kwa kiasi kikubwa. Kampuni ya Huawei ndiyo iliyojejenga mkongo huo.



Alisema kwa kuanzia mradi huo utazihusu shule 50 ambapo shule mbili kutoka kila mkoa zitaunganishwa kwenye mtandao saa zote (ziko online) zikiwa na madarasa ya kujifunzia teknolojia mpya (multimedia classrooms), maabara ya kompyuta (computer lab),  projekta, mafunzo ya kwenye mtandao yanayofundishwa kwa njia ya video, (Online video teaching) na (online applications).



“Shule nyingine 100 zimekwishaainishwa lakini zenyewe zitakuwa zikipata mafunzo offline (hazitakuwa mtandaoni moja kwa moja), bali katika awanu ya pili zinaweza kuunganishwa na kuwa online kutegemea na upatikanaji wa intaneti na kasi yake,” alisema.



Alisema shule hizi zitakuwa zikipokea mawasiliano kutoka kituo chao kikuu ambacho kimejengwa Dakawa, Morogoro.Vilevile Bw. Xu alimkabidhi Waziri Mkuu hati ya makabidhiano ya msaada wa dola za marekani 155,000 kwa ajili ya ujenzi wa ujenzi wa madarasa mawili na vifaa vya komputa kwa shule ya msingi Kibaoni ambayo alisoma Waziri Mkuu iliyoko wilayani Mlele, Katavi.



Akitangaza matumizi ya msaada huo, mtaalamu kutoka kampuni ya Huawei, Bw. Moses Hella alisema msaada huo utatumika kujenga madarasa mawili moja likiwa computer lab na jingine ni darasa la kujifunzia teknolojia mpya (multimedia classroom), kompyuta 50, laptop tano kwa ajili ya walimu, Huawei tablets 100 na audio system.Kwa upande wake, Waziri Mku aliishukuru kampuni hiyo kwa kukubali kutumia teknolojia yake katika kuendeleza elimu nchini kwa kuanzisha mfumo wa E-Education kwenye shule 50 kwa wakati mmoja.



Aliishukuru pia kampuni hiyo kwa kukisaidia Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela cha Arusha na kuongeza kuwa angependa  kuona chuo hicho kinakuwa cha mfano katika maeneo ya utafiti na teknolojia ya mawasiliano barani Afrika.Kuhusu msaada kwa shule ya msingi Kibaoni, Waziri Mkuu aliwashukuru kwa kumuunga mkono katika kampeni yake ya kuhakikisha amefanya kitu kuisaidia shule hiyo ambayo alisoma kati ya mwaka 1957 na 1960.



“Ninawashukuru sana kwa msaada huu. Niliahidi kwamba kabla sijaondoka madarakani nataka nifanye jambo la ukumbusho kwa manufaa ya jamii ya eneo lile. Kwa kweli nawashukuru sana kwa kutupatia msaada huu naamini kuwa shule hii sasa ni ya kisasa na wanafunzi wake watakuwa na elimu ya teknohama na siyo wa BBC (born before computers) kama mimi.



Alisema ataikabidhi hati hiyo kwa viongozi wa Halmashauri yake ili watunze kwenye rekodi zao.Shule ya msingi Kibaoni aliyosoma imechakaa, eneo ilipo ni dogo sana na haifai kwa ukarabati. Ili kukamilisha azma yake,  Waziri Mkuu aliomba Halmashauri ya Wilaya ya Mlele itafute eneo jipya ili ujenzi wa shule hiyo ukikamilika, wanafunzi walioko katika shule hiyo wahamie kwenye shule mpya. Hadi sasa madarasa 12 yamekwishajengwa na kuezekwa.



Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya sita ya ziara yake ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya China leo asubuhi amewasili Chengdu ambako atakuwa na mikutano mbalimbali.


IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATATU, OKTOBA 21, 2013

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. KWA HIYO KILA KIONGOZI AKIAMUA KUSAIDIA SHULE ALIYOSOMA, SISI AMBAO SHULE HAWAKUSOMA VIONGOZI NDIO ZIWE ZERO?

    ReplyDelete
  2. kwa wle wasiojua, hii ni kampuni bingwa duniani iliyoweza kuweka mitamboa mipya ya simu za mkononi 4G hapa Ulaya. Ilikuwa pia na mkataba wa kuweka mktambo hiyo ya kisasa marekani lakini wa marekani wakawashtukia kuwa wanaweza kufanyia upelelezi wa mazungumzuo yao.
    kwa maneno mengine,ni dhana potofu kudhani kuwa kitu toka China ni dhaifu. hawa wenzetu wanazidi kupe duniani, kiuchui, kiteknolijia na kielimu.
    tunazidi kuwashukuru kutuletea maendeleo Afrika..angalia barabara, mashule nk..

    Mdau ugahibuni

    ReplyDelete
  3. Wajanja watazila tu! dola 155, 000 zinatosha kujenga madarsa kadhaa na vifaa vya kutosha lakini yetu macho! Tamaa na uchoyo umejaa! Hata ungempa nani nafasi watu wanafikiria kujinufaisha badala ya kuleta maendeleo ya nchi! Sijui hii simu watu waliipata wapi!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...