Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiongea na waandishi wa habari mapema leo kwenye ukumbi wa mkutano wa Wizara ya Mambo ya Nje, jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Balozi Rajabu Gamaha, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje. 

Waandishi wa habari waliokusanyika kumsikiliza Mhe. Waziri Membe. 

Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ukijumuisha Balozi Irene Kasyanju (kushoto), Mkurugenzi wa Kikengo cha Sheria, Balozi Simba Yahya (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Mbelwa Kairuki (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia na Balozi Dora Msechu (wa nne kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika. 

Wengine waliohudhuria Mkutano huo ni Bw. Mkubwa Ally (kushoto), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Thobias Makoba (katikati) na Bw. Togolani Mavura (kulia), Wasaidizi wa Mhe. Waziri Membe. 

Kwenye Mkutano pia alikuwepo Bw. Kaaya (wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa  

Mmoja wa waandishi kutoka gazeti la The Citizen, Bw. Mkinga Mkinga akiuliza swali kwa Mhe. Waziri Membe.  

Mhe. Waziri Membe akifafanua ombi la Kenya kuhusu uhalali wa kuwafikisha Viongozi Wawili wa juu wa Serikali ya Kenya kwenye Mahakama ya Kimatafa (ICC) kujibu Makosa ya Jinai. Kulia ni Balozi Rajabu Gamaha na kushoto ni Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 

Wakurugenzi wakisikiliza kwa makini maswali mbalimbali yaliyokuwa yakiulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani).  Kulia ni Bw. Mndeme, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, na Bw. Ligaganya, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango.

Mhe. Waziri Membe akihojiwa na Bw. Erick David Nampesya, Mwandishi/Mtangazaji wa Shirika la Habari la BBC. 

Na TAGIE DAISY MWAKAWAGO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb), akutana na waandishi wa habari leo kujadili uhalali wa kuwafikisha Viongozi Wawili wa juu wa Serikali ya Kenya kwenye Mahakama ya Kimatafa kujibu Makosa ya Jinai. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje, jijini Dar es Salaam.
Waziri Membe alikuwa akielezea yaliyojiri kwenye Kikao cha dharura cha Viongozi Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (UA) kilichomalizika mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia jana tarehe 12 Oktoba, 2013.  Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mfalme Mswati wa III, Rais wa Swaziland, na Viongozi Wakuu na Watendaji Wakuu wa Serikali barani Afrika.

Kikao hicho kiliitishwa kutokana na ombi la Serikali ya Jamhuri ya Kenya ya kutaka UA kujadili mahusiano yaliyopo kati ya nchi za Afrika na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) na iwapo ni sahihi kwa Viongozi Wakuu wa Nchi za Afrika kufikishwa katika Mahakama hiyo kujibu mashtaka wakati wakiwa madarakani.

“Viongozi hao wa Afrika waliazimia mambo makuu matano,” alieleza Waziri Membe, huku akiyataja mawili kuwa hakuna Kiongozi yoyote kutoka barani Afrika atakayepelekwa ICC au Mahakama yoyote kujibu mashtaka wakati akiwa madarakani hata akiwa anashika nafasi ya kukaimu. 

Mengine ni kuwa mashtaka yanayomkabili Kiongozi yoyote barani Afrika yasubiri hadi Kiongozi huyo atakapomaliza muda wa uongozi wake.  Aidha, Mhe. Waziri alieleza kusikitishwa kwa Viongozi wa Afrika na namna Mahakama ya ICC inavyoendesha shughuli zake kwa kile walichokiita “kuwaandama Viongozi wa Bara la Afrika kuliko Viongozi wa Mataifa mengine hata pale panapokuwa na ushahidi wa Viongozi hao wengine kufanya makosa ya Jinai.”

Waziri Membe alihoji inakuwaje kwamba kati ya kesi 30 zilizopelekwa ICC tangu mwaka 2004, ishirini na saba (27) zinatoka barani Afrika.  “Haya yote yalijadiliwa kwa kina, pamoja na pendekezo la kujitoa kwenye uanachama wa Mahakama ya ICC,” aliongeza Waziri Membe.
Alisema suala la kujitoa uanachama wa ICC limeachiwa kila nchi kuamua, ingawaje linategemewa kujadiliwa tena katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wa Sheria wa nchi wanachama wa mahakama hiyo kitakachofanyika tarehe 29 Novemba mwaka huu nchini Uholanzi. Hivi sasa kuna nchi thelathini na nne (34) barani Afrika ambazo ni wananchama wa Mahakama hiyo.
Akiendelea kuzungumza katika Mkutano wake wa leo na waandishi wa habari ambao pia ulihudhuriwa na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Membe amesema kuwa Umoja wa Afrika umepeleka ombi lake rasmi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kuahirisha kesi inayowakabili viongozi hao wa Kenya.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Membe alitumia fursa ya mkutano wake na waandishi wa habari kutoa salamu za pole kwa Bibi Ufoo Saro, Mwandishi/Mtangazaji wa kituo cha televisheni ITV, na familia yake, kufuatia  taarifa iliyomfikia kuwa Bibi Saro amelazwa hospitali akiwa mahututi baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya. Mama yake mzazi, Anastazia Saro na mtoto wake waliuwawa katika shambulio hilo.  Taarifa zinasema mtuhumiwa ni   mchumba wa Bibi Saro, ambaye anadaiwa kufyatua risasi kwa familia hiyo na hatimaye kujipiga risasi na kufa.
Sambamba na taarifa hiyo, Mhe. Waziri Membe pia aliwatakiwa wananchi sikukuu njema ya Kumbukumbu ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambayo itaadhimishwa Kitaifa kesho tarehe 14 Novemba 2013.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 14 mpaka sasa

  1. Kusubiri hadi viongozi waharifu waondoke madarakani sio! Hilo nalo neno. Sheria iliyounda ICC inasemaje? Changamoto ipo katika hili kwa sababu ni vigumu watu waliotendewa uhalifu na kuuwawa kwa ndugu zao kuona aliyewaua ndugu zake anaendelea kudunda mitaani na anatawala. Sheria inaweza kumpa muda mkosaji au hata mkosaji wa kawaida asiye na madaraka ya Urais nafasi ya kuendelea kupeta tu? Hili ni suala la kisheria zaidi, kwa maoni yangu. Sheria ni msumeno ndugu zangu.

    ReplyDelete
  2. All of them should be sent to ICC, not only for exploiting their citizens but also for the monies they have hidden in Uswiss and other countries.

    Mnaogopa nini kama hamna makosa?

    ReplyDelete
  3. VIONGOZI WA AFRIKA WOTE MNABIDI MUONE AIBU, MNAJITENGENEZEA MAZINGIRA YA KUTOSHITAKIWA MKIFANYA MAKOSA!!!

    HAKUNA KUJITOA ICC NA HAKUNA KUWATETEA MAANA WOTE WALIFANYA MAKOSA KABLA HAWAJAKUWA MARAIS...NA ATA KAMA NI MARAIS NA WAMEFANYA MAKOSA WANATAKIWA KUSHTAKIWA!!! WAJANJA HAO NDIO MAANA WALIGOMBEA URAIS KWA NJIA YA KUKIMBIA MAHAKAMA.

    NO EXCUSE KAMA WAMEFANYA MAKOSA WAPELEKENI MAHAKAMANI HAKUNA KUJITETEA PERIOD!!

    ReplyDelete
  4. Sheria gani inamwacha mhalifu kisa ni kiongozi mkubwa? Waafrika tulisaini wenyewe huu mkataba, hivi tuliposaini tulidhani nani wa kushakiwa ICC!!!

    ReplyDelete
  5. Nakubaliana na wadau wote hapo juu,maana justice delayed is justice denied. Waende hap chap wakamalizie kesi zao huko, hamna kusubiri hadi watoke madarakani, si walijua haya yanaweza tokea wakiwa viongozi.Na wakenya kama "kweli" waliwachangua watu hawa kama viongozi walifanya hivyo wakijua kabisa wana case, walitahadharishwa juu ya hilo, kazi kwao kama walichangua viongozi kwa misingi ya "ukabila".

    Hamna TZ kujitoa kwenye ICC, watanzania tutapinga hilo vikali, hapa tu ICC ipo hali mbaya mijitu inajiona iko above the law sasa na hiyo ICC isipokuwepo si itakuwa majanga.

    ReplyDelete
  6. i smell a big raaats.

    ReplyDelete
  7. Huyu Membe nae asituambie ujinga hapa, huo ni upuuzi akawaambie hayo maneno hao anaowaita marais wa kiafrika. Wezi tu hao na wauaji kwa hiyo watu watakuwa wanaua kisha wanakwenda kujikinga kwenye urais ili wasishitakiwe mpaka wamalize urais sio? huo ni ujinga ambao hatuutaki kwa sasa hapa afrika.

    ReplyDelete
  8. Mimi nashindwa kuwaelewa hawa viongozi wa africa sijui wamerogwa na nani,mfnatoa mifano miwili tu:1,charles Taylor wa Liberia,Bagbho wa Ivory coast hao tu wawili waliua watu wangapi?,viongozi wa africa wasitudanganye ICC acha iendelee kuwepo ili wakituua kwa uroho wa madaraka wakaonje joto ya jiwe,hata hawa Uhuru na Ruto ni wauwaji acha mahakama ifanye kazi yake na mwisho wa siku wahukumiwe

    Simpo.

    ReplyDelete
  9. Hakuna mahakama local inaweza kuwashitaki viongozi na haki ikatendeka; tofauti na nchi za western ambako at leats hakuna wa kuogopa...ICC ndio mkombozi wetu sisi Waafrica...Kenya walikuwa na muda wa kuwashitaki wahalifu wao locally; did they do that??????

    Stop being selfish...naungana na mdau kama hauna kosa ICC mnaiogopa ya nini????

    Afu naona Tz tunafuata mkumbo...kuna nchi jamani viongozi wao ni majanga...sisi hatuwezi kujua siku za usoni...ila kwa sasa why so much worry...mnasapoti madikteta

    ReplyDelete
  10. wewe muheshimiwa Membe na genge lenu acheni kuleta mambo ya kiusaniii..huyo kenyata na mwenzake wanajua walichokifanya ndiyo maana mahakama inawashitaki sasa kama hamna cha kuficha kwaninin mnaogopa..madikiteta siku wanakuwa waoga wa kuadhibiwa.....askofu Desmond Tutu alisema juzi kuwa 'kuna baadhi ya viongozi barani afrika wanajiona wao miungu mitu' Yaani membe maovu yote na maaafa yote ya wakenya walioteketea ktk zile ghasia wewe haikusumbui hata kidogo ? au yale maafa ya watu wa Darfu wewe Membe na genge lenu hilo haliwasumbui hata kidogo ? !! Aibu kubwa kuendelea kutetea maovu na udhalilishaji wa haki za binadamu..Viongozi wa Afrika wanaongoza kushitakiwa kwa sababu wanaongoza katka maovu ya raia wao..That is why !! Mtu anaandamana kwa amani na bendera nyepe wewe unatuma ffu na risasi za moto !! sasa kwanini usiplekwe the HAGUE !! Badilikeni na muwe na mapenzi ya kweli kwa mnaowatawala na hamtakuwa na hofu hata kidogo na ICC...waacheni Kenyata, Albashir na magenge yao wakachezee mziki wa ICC...Mziki mrefu kweli...kama vile mziki wa marehemu Makiadi...waambieni wamuuilize mwenzao aliyewatangulia Ndugu Charles Tylor....Asante bwana Michuzi...

    ReplyDelete
  11. NAWAUNGA MKONO WADAU HAPO JUU, VIONGOZI WA AFRIKA NA KOTE KULE WANA BIDII YA KUFANYA MAZINGIRA AMBAYO YATAWALINDA WANAPOFANYA UFISADI WAO, HII ICC ILIPOKUWA INAUNDWA HUKO ROME, VIONGOZI WETU WALIKURUPUKA TU KAMA KAWAIDA YAO KUSIGN HICHO WALICHOSIGN BILA KUJUA ATHARI ZAKE, MAANA WANGEKUA NA AKILI HIYO WASINGESIGN, MAANA MATAIFA MENGINE TENA HAYO YANAYOITWA YAMEENDELEA NA WATIMIZA HAKI ZA BINAADAM WALIKATAA KUSIGN, LAKINI MAMBUMBU WA AFRIKA BILA KUJIULIZA KWANINI HAWA WALIONZISHA HILI JANGA WAO WANAKATAA KUSIGN? BILA KUPOTEZA MUDA NASEMA HIVI HATOKI MTU ICC, LEO MNAJITIA HAMTAKI, KESHO KIKITOKEA AMBACHO MTAIHITAJI ICC, MTAJIUNGA TENA? FANYENI KAZI KWA UADILIFU, BASI ICC HAITAHITAJIKA, LAKINI KWA HAYO MABAVU YENU NA UFISADI WENU BASI MJUE ICC MNAYO HIYO. VIVA ICC

    ReplyDelete
  12. Wapelekwe wapi? Na si mlisaini wenyewe? Au mlilazimishwa?! Kwa nini hamkutafakari repurcasion ya maamuzi yenu?!

    Katika hali hii, mtu akifanya uhalifu, atafanya kila liwezekanalo ili awe kiongozi wa nchi ili sheria ipite pembeni!

    Na kwani wamehukumiwa? Si wanaenda kujitetea kama hawahusiki na unyama uliofanyika si wanarudi wanaendelea na kazi ya kuwatumikia wananchi?!

    Unajua hizi sheria hazitakiwi kuangalia personality! Huyu wa Sudan wakati anasakamwa AU haikukutana kuongelea hili!

    Na hizi ni double standards!! Sikusikia sauti ya pampja ya nguvu ya kulaani Kiongozi aliyeiokoa hiyo AU alipofanyiwa unyama na kuuawa. Zaidi tu yalikuwa manun'guniko. Hapa tunaenda UN tunashindwa kulaani hicho kitendo!!

    Poor Africans, hatujapata viongozi wa kutetea maslahi yetu, bali ni club ya kuangalia maslahi yao!! Thomas Sankara uko wapi!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  13. Yaani Waafrika tukiitwa wajinga tukubali tu! Yaani tunateteta maovu ndio maana hatuwezi kuendelea! Kama majamaa wameharibu wathibitiwe! Mnapoteza hela kukaa na kutetea uovu! Mbona msepeke hizo hela kwa waathika wa hayo mauaji waliosababisha! Haya majamaa bangi tupu!

    ReplyDelete
  14. This is very fishy indeed. Nawaunga mkono wadau wote hapo juu. I couldn't put it better myself. I did not realize that we had some blatantly dodgy characters in high places. I do hope all leaders do read the comments and take on board the comments of true African citizens. Mungu ibariki AFrica na viongozi wake. HAKI ,UMOJA na AMANI is an anthem with deep meaning nd message. Our leaders need to recite this and put into practice the message within.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...