Na Anna Nkinda – Maelezo

Dar es Salaam, Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kesho anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za mahafali ya kwanza ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo kijiji cha Nyamisati wilayani Rufiji mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambayo ndiyo inamiliki shule hiyo Daudi Nasib inasema jumla  ya wanafunzi wa kike 67 wanatarajia kuhitimu elimu yao ya kidato cha nne Novemba mwaka huu.

Taarifa hiyo inasema shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama  ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Taasisi ya WAMA na wadau mbalimbali wa maendeleo  kutoka ndani na nje ya nchi wenye mapenzi ya kusaidia jamii. Bodi ya Wakurugenzi ya WAMA iliamua Shule hiyo iitwe jina hilo kwa heshima ya Bwana Hayao Nakayama  kutoka Japani aliyetoa msaada uliosaidia ujenzi wa awamu ya kwanza ya shule.

“Moja ya malengo ya  Taasisi ya WAMA ni  kusaidia upatikanaji wa Elimu bora ya Sekondari kwa watoto wa kike na watoto wengine waishio katika mazingira hatarishi na yatima. Na ni kwa mantiki hii ndiyo maana shule ya WAMA- Nakayama imejengwa ili  kutimiza lengo hili.

Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA,Mama Salma Kikwete na Bodi ya Wakurugenzi  ya WAMA inapenda kutoa shukrani za dhati kwa wadau wote wanaosaidia Shule ya WAMA- Nakayama na kuunga mkono juhudi za Taasisi yetu”, ilisema taarifa ya Nasib.

Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama ilianza mwaka 2010 ina  wanafunzi wa kike 325 kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambao ni yatima na wengine wanatoka familia maskini, watoto hawa  wasingeweza kupata elimu ya sekondari bila ya  msaada wa  Taasisi ya WAMA  ambayo huwapatia mahitaji yao yote bure ikiwemo; malazi, chakula, sare za shule, shajara, vitabu na nauli za kwenda makwao kipindi cha likizo.


Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ni Taasisi isiyo ya kiserikali na  isiyo ya kibiashara iliyoanzishwa na Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, mwaka 2006 ina malengo ya kuboresha  maisha ya wanawake na wasichana  katika  masuala ya afya, elimu na uchumi pamoja na kutengeneza fursa za maendeleo ya wakina mama na watoto.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Aina yoyote ya uwekezaji unaowapa nafasi na matumaini watu ambao kwa namna nyingine wasingeweza kutoka ki-maisha nauunga mkono kwa dhati kabisa....Hengera Ho. JK kupokea mwaliko huu nadhani utawatia moyo zaidi WAMA kusidi kuwekeza kwenye maeneo ya huduma za jamii ikiwemo elimu n.k.& Hongera WAMA kwa kuwafikia watoto wetu wa kike kielimu; nadhani kwa njia hiyo mtatutengenezea akina "Asha-Rose" wengine huko mbele ya safari!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...