SERIKALI kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wiki iliyopita ilitoa pongezi kwa waandaaji wa Tamasha la Pasaka, kampuni ya Msama Promotions  kuhusu ubora wa tamasha la mwaka huu na kuwataka waandaaji hao kuendeleza mipangilio hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa kupokea ripoti na kutathimini tamasha la mwaka huu lililofanyika kwenye mikoa mitano hapa nchini  kwa lengo la kuboresha matamasha  ya Pasaka yajayo, Mkurugenzi wa Ukuzaji  Sanaa wa Basata, Nsao Shalua pamoja na kupongeza jitihada na mipango inayofanywa na Msama.

Shalua aliongeza kuwa michango inayotolewa na kampuni hiyo kwa jamii  kupitia matamasha hayo ni mfano wa kuigwa na kuwasihi wadau wengine kushiriki na kuchangia katika kutunisha mfuko wa matamasha ya Pasaka.

Ofisa Sanaa Mkuu, Philemon Mwasanga alitoa wito kwa Msama mbali ya kujenga kituo cha kulelea watu wenye uhitaji maalum ambao ni wajane, walemavu na  Yatima  kitakachokuwa nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam wawe na mkakati maalum wa kuvumbua na kuibua wasanii wachanga katika tasnia ya muziki wa injili hapa nchini kwa sababu muziki wa sasa umemezwa na teknolojia.

Mwasanga aliwataka waandaaji hao kuazimia kuanzia mwakani kuacha matumizi ya CD wawapo jukwaani ili kuuokoa muziki ambao unapoteza mwelekeo wake hasa Kimataifa.

Aidha Mwasanga alitumia fursa hiyo ya kumsihi Msama kununua vyombo vyake vya muziki ili kufanikisha matamasha  yake  ili waimbaji waonyeshe vipaji vyao katika tasnia ya muziki.

“Ili  kuendana  na kasi ya muziki  katika hadhi ya Kimataifa, unaweza kutakiwa nchi za wenzetu,   ili ukidhi inatakiwa kujipanga kimataifa katika utayarishaji  na sio matumizi ya (mshindo nyuma) CD,” alisema. Mwasanga alisema mtindo huo umepitwa na wakati, waimbaji wanatakiwa wazoeze kumiliki jukwaa kwa kuimba na kupiga moja kwa moja.

Ofisa Matukio wa Basata, Kurwijira Maregesi alisema matamasha yajalo Msama iwe mfano wa kuigwa kinidhamu na muonekano wa mavazi kwa waimbaji.

Maregesi alisema waimbaji wanaume wajiepushe na uvaaji wa herein masikioni, kusuka nywele na kuvaa suruali chini ya makalio kwa kuwa muziki wa injili unamtukuza Mungu.

Maregesi alitoa wito kwa kampuni hiyo ambayo ina changamoto ya udhamini na kueleza kuwa wana bahati kubwa kuendelea na utaratibu wa uandaaji wa matamasha ya Pasaka bila kutetereka kwani  baadhi ya waandaaji wameshindwa kuendelea kutokana na changamoto ya kukosa wadhamini.

Alisema ili wadhamini waendelee kukuthamini inatakiwa wakukute na cha kwako, kama wakikupa kitu wasikimbie mapema kwa sababu unacho cha kwako,  hivyo Msama asibabaike na wadhamini.

“Usitegemee mtu mwingine kukuendeshea nyumba yako, wadhamini wetu wamezoea kuona mambo yao yanafanyika, yasipofanyika kama wanavyotaka wanajitoa,” alisema Maregesi.

Maregesi aliwapa mwangaza Msama kwa kuendelea kuwafuatilia wadhamini kwa sababu tamasha lao ni la Kimataifa na kuwataka waendelee na mikakati hiyo ya maendeleo.

Ili kunogesha tamasha lijalo, Ofisa wa Basata, Vick Temu alipendekeza kuwepo kwa Projector zitakazofungwa uwanjani ili kuwapunguzia bughudha watazamaji watakaoukuwa mbali na jukwaa Kuu.

Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo kupitia Makamu Mwenyekiti wake, Abihudi Mang’era alitoa pongezi kwa  Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ambayo matamasha ya Pasaka yalifanyika licha ya fununu za  matishio ya ugaidi zilizosambazwa.

Mang’era  alisema tamasha lijalo litakuwa la kimataifa zaidi kwa sababu litaongeza idadi ya mikoa na waimbaji wa Kimataifa ambapo lina malengo ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kuingia nchi za jirani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...