Mke wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, (CCM), kutoka Lindi, Mama Salma Kikwete akipokewa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Lindi Ndugu Ali Mtopa wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Lindi tarehe 24.11.2013.
Mjumbe wa NEC Taifa ya CCM, Mama Salma Kikwete, akivishwa skafu mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Lindi tarehe 24.11.2013.
Mjumbe wa NEC Taifa ya CCM kutoka Lindi Mjini na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongea na wajumbe wa Halmashauri ya Tawi la Jangwani lililoko katika Kata ya Chikonji huko Lindi terehe 24.11.2013.
Mke wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kutoka Lindi Mjini Mama Salma Kikwete akisononeka baada ya kubaini kuwa watoto wengi wanaoonekana katika picha kutoka Kijiji cha Jangwani wamekatisha masomo yao. Mama Salma alikwenda kijijini hapo kuongea na wajumbe wa Halmashauri ya Tawi hilo tarehe 24.11.2013 PICHA NA JOHN LUKUWI.

Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi

Wazazi mkoani Lindi wametakiwa kusimamia  elimu ya  watoto wao kwa  kufuatilia mahudhuria yao shuleni jambo ambalo  litawasaidia katika maisha yao ya baadaye kwa kuweza kujiajiri au kuajiriwa pindi watakapomaliza masomo na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Taifa (NEC) wakati akiongea  kwa nyakati tofauti  na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho  katika matawi ya  Jangwani, Tandangongoro na Mkupama yaliyopo katika wilaya ya Lindi mjini.

Akiwa katika tawi la Jangwani lililopo katika kata ya Chikonji Mama Kikwete aliongea na  watoto ambao aliwaita ili awasalimie na baada ya kuwauliza maswali kuhusu elimu walisema baadhi yao  waliacha shule kwa ajili ya utoro. Jambo alilolifanya ni   kuwasisitiza watoto hao kusoma kwa bidii na kuepukana na tabia ya utoro kwani elimu ni ukombozi wa maisha yao.

Baada ya kuongea na watoto hao ambao wengi wao walikuwa ni wanafunzi wa shule ya Msingi Mjumbe huyo wa NEC taifa aliongea na viongozi wa CCM na kuwataka wao kama wazazi  kutatua tatizo  la utoro kwa watoto wa kijiji hicho  kwa kusimamia na kuhakikisha wanakwenda shule kwa wakati.

“Hali ya elimu katika mkoa wa Lindi ni ngumu vijana hawasomi wengi wao wanakatiza masomo kwa ajili ya utoro na kuolewa sisi kama viongozi ni  lazima tupige kelele ili kuhakikisha watoto wanakwenda shule na kuhudhuria masomo darasani”, alisema Mama Kikwete.

Aidha Mama Kikwete pia aliwaasa viongozi hao  wa Halmashauri kuu ya tawi kutunza amani iliyopo na kuitumia katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kulima mazao hasa yanayohimili ukame ikiwa ni pamoja na  mtama ili kuepukana na tatizo la njaa linaloikabii wilaya hiyo mara kwa mara.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi Mzee Ali Mtopa alisema katika mikoa ya Kusini ambayo ni Lindi na Mtwara hivi sasa kuna maeneo matatu yanayotoa  gesi ambayo inaleta utajiri  lakini uchimbaji wake unahitaji vijana waliosoma.

“Uchimbaji wa gesi unahitaji kupata wataalam ambao wamesoma kama watoto wetu hawatakuwa na elimu watakuja watu kutoka mbali na kufanya kazi ya uchimbaji wakwetu wataishia kufanya kazi ya vibarua tu. Nawaomba  muwaache watoto wasome msiwaoze au kuwaacha wanakatiza masomo kwa ajili ya utoro”, alisema Mzee Mtope.

Mama Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alikutana na viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Ujumbe wa kuhamasisha kusoma ni muhimu ili tuweze kuchukua ajira kwenye maeneo yetu. Ukiona hata nchi za kiarabu nazo zimeanza kufukuza wahamiaji waliokuja kutafuta kazi hili lituhamasishe kutengeneza ajira zetu wenyewe kwa wingi kabisa katika sekta mbali mbali ikiwemo binafsi. Tusome mkulima aliyesoma ni bora kwa kuelewa mambo, kuchangamkia fursa, na kujiendeleza kuliko asiyesoma.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...