Mwezi uliopita nililazimika
kwenda Kituo cha Polisi cha Osterbay
kutimiza masharti au sheria inayohitaji gari kukaguliwa kila mwaka kama
taratibu za usalama barabarani. Hii haikua mara yangu ya kwanza kufika kwenye
kituo hiki kwani nimekua nikifanya hivi karibu kila mwaka.
Nilipokua naelekea
zilipo ofisi za Usalama barabarani ambazo ziko nyuma ya jengo kubwa la kituo,
nikashangaa kuona mabadiliko makubwa ya mwenekano wa majengo ya kituo kile. Niliona
ukarabati mkubwa uliokuwa unaendana na majengo kupakwa rangi. Nilipofika nyuma
ya jengo nilikuta jengo dogo ambalo ndilo lina ofisi za Usalama Bararani nalo likiwa
limebadilika na ofisi imehamishwa kwenye chumba kilichokua chatumika awali.
Mshangao wangu uliendelea nilipoingia ofisini na kukuta maasifisa wa polisi
waliokua mule ndani wamekaa kwenye ofisi safi na zenye samani (furnitures)
mpya, safi na za thamani kama zilizo kwenye ofisini nyingine za kisasa.
Sikuweza kumuuliza yeyote
juu ya mabadiliko yale na ndani mwangu nikajisemea kuwa ni nafuu kama polisi
wameona umuhim wa kuboresha majengo yao na kuyafanya yawe na mvuto. Baada ya
kumaliza kilichonipeleka, niliamua kuangalia kwa karibu bango linaloonesha
ujenzi unaondelea ili nijue ni nani anafanya ukarabati ule. Kwa mshangao
mkubwa, macho yangu yaligongana na Jina la kanisa la CHRIST EMBASSY TANZANIA ambalo
pia linaitwa LOVE WORLD kwenye kibao kile kama mfadhili wa ukarabati ule. Kwa
maana nyingine kanisa la CHRIST EMBASSY
TANZANIA ndio wamejitolea kukarabati KITUO
CHA POLISI OSTERBAY.
Nilivutiwa sana na kibao
kile na nikatamani nikipige picha ili nikaitumie nitakapoamua kuweka jambo lile
kwenye maandishi. Lakini nikashtukia kuwa niko kwenye himaya ya usalama na kama
ningetimiza haja ya moyo wangu huenda ningeshtuka baadaye sana nikiwa selo
baada ya kupata mtikisiko wa ubongo (concussion) ambao ungekua umesababishwa na “mitama ya mfululizo” ambayo ningeipata hata
kabla sijamaliza kupiga picha ya kwanza.
Nilitiwa moyo sana na
kitendo hiki cha dhehebu la dini kujitolea kukarabati kituo cha polisi. Sina
hakika kama walifanya hivi kwa kuombwa au kwa kukusudia wao wenyewe, lakini
kwangu niliona ni aina mpya ya jinsi madhehebu ya dini na hasa kanisa kuonesha
upendo wa kubadilisha maisha ya wengine kwa vitendo.
Kilichonigusa zaidi kwa
msaada huu ni ukweli kwamba vituo vingi vya polisi kote nchini, ni kati ya
majengo ya umma ambayo kwa sehemu kubwa
yako katika mazingira duni, machafu, na yasiyo a mvuto kabisa jambo ambalo
linavifanya visiwe rafiki sio tu kwa waonkwenda kutafuta huduma bali hata kwa
polisi wenyewe wafanyao kazi humo. Huenda hali hii ya majengo na mazingira ya
vituo vya polisi ndiyo imefanya watu wengi kutopenda kabisa kufika katika vituo
vya polisi maana mazingira yake hayaoneshi kuwa ni maneo rafiki na salama kwa
anayekwenda kutafuta haki, kulazimika kutoa haki kwa wengine au kuwajibika kwa
matendo yao.
Huenda mazingira haya ndio yanawafanya askari polisi wengi kutokua
rafiki kabisa na raia na wenye jazba na hasira muda mwingi kwa vile mazingira
ya kazi yanayowazunguka hayawaoneshi kuwa ni watu wa thamani na kazi yao ina
heshima na hivyo kulazimika kutumia njia nyingine kujitafutia heshima.
Kwa wale waliojifunza
manejimenti hasa katika nadharia (concepts) za hamasa (motivations) zinazoweza
kumfanya mfanyakazi au mtumishi kutimiza wajibu wake vizuri, wanafahamu kuwa
sio ukubwa wa ujira/mshahara pekee unaochangia hamasa bali kuna mambo (factors)
mengine ambayo yako kisaikologia, kiutu na kitamaduni zaidi. Kuthibitisha hili, unaweza kuona baadhi ya watu
wanaacha kazi nzuri zenye cheo au kipato kikubwa katika kampuni, shirika au
hata katika taasisi za serikali kwa kigezo cha kutoridhika na mazingira ya
kazi.
Ndio mana ni rahisi kusikia
matapeli wakidanganya watu kuwa wao ni maafisa wa usalama wa taifa, wako TRA au
BOT na sio maafisa magereza, fire au makarani wa mahakama. Hamasa ya kazi na
kuipenda kazi vinachangiwa sana na mazingira ya ofisi au eneo la kazi kuwa na
mvuto unaotokana na thamani ya ofisi yenyewe na samani zilizoko, usafi wa ofisini na eneo ofisi ilipo. Ndio
mana ni rahisi kumsikia mtu hata isivyo kweli kuona fahari kusema ofisi yake
iko Posta au Masaki kuliko aseme anakwenda ofisini Tandale au Mburahati.
Nawapongeza sana uongozi na
kanisa la Christ Embassy Tanzania kwa
ufunuo huu wa kuboresha mazingira ya kituo cha polisi. Kazi yenu ni kubwa
kwani hamujasadia tu kufanya majengo yawe na mvuto, bali mumewasaidia maafisa
na askari wafanyao kazi katika kituo hiki kuona na kujisikia kazi yao ni ya
muhim, yenye thamani na ya heshima na hivyo kuongeza hamasa ya utendaji kazi
wao katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao huku wakitenda haki.
Kuna
tofauti sana ya utendaji kazi kati ya askari anayetoka nyumbani kwenye kazini
huku akiwaza kuwa zaidi ya bunduki, ofisi yake ina tiles chini, ina ukuta msafi
na anakalia kiti cha kuzunguka; ukimlinganisha na yule anayewaza bunduki iliyo
kwenye ofisi chafu, isiyo na ukuta msafi na yenye kiti cha mbao kichafu, kibaya
na wanachokalia kwa kupokezana kutegemeana na nani alitangulia kukaa.
Nawatia moyo madhehebu
mengine ya Kikristo na dini zingine, kuiga mfano huu mzuri wa Christ Embassy wa
kusaidia maeneno yanaoonekana sio rafiki kwa jamii kama Polisi. Kama kila
kanisa katika eneo lililoko likijotolea kukarabati au kujenga vituo vya polisi,
ni wazi dhana nzima ya POLISI JAMII itakua imeongezewa nguvu kwa namna ya
kipekee na MATOKEO MAKUBWA SASA ya kiusalama yatakua dhahiri kwa kila mmoja.
Mwalim
MM
mathewmndeme@gmail.com
Nashukuru Mwalimu MM kwa kulileta hili katika hadhira yetu. Ni wakati wa kubali mtazamo wa mambo kadha wa kadha yanayotuzunguka na pengine kutuhusu badala ya kusubiri serikali kufanya kwa ajili yetu. Mitazamo chanya hujenga fikra chanya na pengine hiyo hupelekea kufanya maendeleo katika nyanja tofauti tofauti. Watanzania tubali mitazamo yetu kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu, unaweza kufanya asilimia 0.01 na mwingine na mwingine na mwingine, baadaye ukizijumlisha unakuta asilimia iliyofanyika ni kubwa kuliko mategemeo. Mungu ibariki Tanzania.
ReplyDeleteKi2