Na Mwandishi Maalum 
 Wilaya ya Karagwe iliyopo katika Mkoa wa Kagera nchini Tanzania, inatarajiwa kuwa na Chuo cha kwanza cha aina yake katikafani ya Uuguzi ( Nursing Collage )kitakachojengwa kwa misaada na ushirikiano kutoka Chuo Kikuu cha Wilkes kilichopo katika mji wa Pennyslavia, nchini Marekani. 
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Professa Evene Estwick wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi. Mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Uwakilishi huo jijini New York. 
Akiwa ameambatana na Dkt. Andrew Cesari ( MD, MBA) ambaye ni msimamizi wa Mganga wa Hospitali Teule ya Nyakahanga wilayani Karagwe ambako chuo hicho kitajengwa , Professa Estwick alimweleza Balozi Manongi kwamba Chuo hicho kinatarajiwa kuwa tayari mwishoni mwa mwaka ujao na kwamba michoro tayari imeshakamilika. 
 Aidha ilibainishwa katika mazungumzo hayo kwamba, wataalamu wawili katika fani ya uuguzi wanatarajiwa kwenda mwakani huko Karagwe kwa lengo la kuangalia namna bora zaidi ya kushirikiana katika eneo hilo. 
Katika mazugumzo hayo ambayo pia yalihudhuriwa na Dkt. Andrew Mayala ( MD, MPH) ambaye ni Medical Officer wa Wilaya ya Karagwe na Bi. Lorienetter Williams ambaye ni Mwanafunzi kutoka chuo hicho, ilielezwa kwamba ujenzi wa Chuo hicho cha Uuguzi unatokana na uhusiano na ushirikiano wa takribani miaka kumi na tatu uliopo kati ya Chuo Kikuu cha Wilkes na Hospitali ya Nyakahanga. 
 Kwa mujibu wa Dkt Andrew Cesari ambaye ndiye mwanzilishi wa fikra hiyo ya kuwa na Chuo cha Uunguzi, alisema kwa kuanzia chuo kitakuwa kinatoa mafunzo ya uuguzi, lakini lengo ni kukipanua kwa kuongeza fani mbalimbali ili kuwapata wataalamu wengi Zaidi. 
“Nilipofika Wilayani Karagwe mwaka 2007, nilikuta wilaya hii ingawa ni kati ya wilaya kongwe nchini, ikiwa haina chuo cha aina yoyote hata cha VETA, ndipo likanijia wazo la kubuni mradi huu, na bahati nzuri marafiki zetu wameonyesha nia ya kutusaidia kufikia lengo hili na mambo yote yakienda sawa ujenzi wa chuo utaanza mwakani”. 
Akielezea umuhimu wa Chuo hicho, Dkt. Andrew Cesari anasema manufaa hayatakuwa kwa kuzalisha wataalamu wengi katika eneo la afya, lakini kitakuwa na manufaa makubwa kwa vijana wengi hasa wale wanaomaliza elimu na kushindwa nini cha kufanya au wapi pa kwenda hasa katika maeneo hayo na ya jirani. 
Kwa hiyo itakuwa ni fursa nzuri kwa vijana wengi kujipatia ujuzi zaidi na kupanua huduma na raslimali watu katika eneo hilo la afya. Anasema Dkt. Cesari 
Dkt. Cesari na Dkt. Mayala walikuwa hapa Marekani kwa mwaliko wa washirika wao yaani Chuo Kikuu cha Wilkes kupitia utaratibu wa kubadilishana wataalamu (exchange program) na wameshiriki katika mijadala mbalimbali ya kitaalam ukiwamo ule uliofanyika katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambapo walipata fursa ya kuelezea uzoefu wao na kubadilishana mawazo na washiriki wengine na pia walifanya ziara katika Chuo kijulikanacho kama Commonwealth Medical Collage kilichopo Scranton. 
Ushirikiano kati ya Chuo Kikuu hicho na Hospitali ya Karagwe ulilanza kwa utekelezaji wa miradi midogo ukiwamo ule wa upelekezaji wa vifaa vya hospitali, ubadilishanaji wa wataalamu na kuwasaidia watoto yatima wanne ambao wamepoteza wazazi wao kutokana na maradhi ya ukimwi. Watoto hao wanne husaidiwa ada na gharama nyingine za shule vikiwamo vitabu kupitia mradi ujulikanao kama “Embrace a Child”, mradi unaoratibiwa na Chuo hicho. 
 Na cha kutia moyo zaidi ni kwamba wanafunzi hao akiwamo Kihinga George wanafanya vizuri kiasi cha kupata nafasi ya kujiunga na kidato cha sita na matarajio yake ni kuwa daktari. “ maendeleo ya watoto hawa ni kati ya hadithi nzuri za ushirikiano wetu, ni watoto wenye akili sana, wanaojituma na walio makini. 
Tunaona matunda yake, hasa kwa kuzingatia kwamba watoto hawa walikuwa hawana msaada wowote tangu wakiwa wadogo” anasema Dr. Evene Estwick kwa furaha kubwa. Kama hiyo haitoshi, gharama za kuwasomesha yatima hao zikiwamo za ada na vitabu zinatokana na michango ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Wilkes kupitia harambee wanazozifanya wao wenyewe. 
Kwa upande wake, Balozi Tuvako Manongi, alielezea kufurahishwa kwake na uhusiano uliopo baina ya Chuo Kikuu cha Wilkes na Hospitali ya Nyakahanga na kwamba ni jambo linalotakiwa kuenziwa na kudumishwa. 
Akasema Serikali inathamini na kutambua mchango wa wadau mbali mbali katika kuchagiza juhudi za serikali za kufikisha huduma za afya karibu na wananchi. Kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ( MDGs) ambayo ufanikishwaji wake wake unahitaji sana ushirikiano kati ya serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi. 
Akabainisha kwamba uboreshaji wa sekta ya afya ni moja ya vipaumbele vya Serikali na hasa katika uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto na kwamba ujenzi wa Chuo cha Uuguzi siyo tu utakuwa unachagia juhudi hizo za serikali bali pia ni ukombozi mkubwa kwa wananchi kutokana na upungufu mkubwa wa wataalamu. 
Aidha Balozi Manongi akasema inatia faraja sana kwamba watoto yatima ambao wanasaidiwa kupitia ushirikiano huo wanafanya vizuri sana katika masomo yao na ni kielelezo kizuri kuwa michango inayotolewa na wahisani inawafikia na kuwanufaisha walengwa na akatoa shukrani zake kwa walimu na wanafunzi kwa moyo wao huo wa kujitolea.
Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi, akizungumza na ujumbe ulioongozwa na  Professa Evene Estwick ( kushoto kwa Balozi) kutoka Chuo Kikuu cha Wilkes ( Marekani) ambacho kinaushirikiano na Hospitapi ya  Nyakahanga iliyopo  Wilayani Karagwe  Mkoani Kagera wengine  ni Dkt. Andrew Cesari aliyeketi kulia kwa Balozi ambaye ni  Msimamizi wa Hospitali hiyo  na anayefuatia ni Afisa  Ubalozi,  Bw. Khamis akifuatilia mazungumzo hayo aidha katika mazungumzo hayo  yupo pia Dkt. Andrew Mayala ambaye ni Medical Officer   wa Wilaya ya Karagwe na Bi. Lorienetter Williams  ambeye ni mwanafunzi kutoka Chuo cha Wilkes.
Balozi Tuvako  Manongi akiwa na  Madaktari Andrew Cesari na  Andrew Mayala kutoka Karagwe ambao walikuwapo nchini  Marakani kwa ziara ya kikazi kwa mwaliko wa wenyeji wako Chuo Kikuu cha  Wilkes kupitia  mpango wa kubadilishana wataalam. wakiwa hapa  Marekani pamoja na mambo mengine walishiriki katika makongamano ya kitaaluma ambapo walibadilishana mawazo na uzoefu na  wenyeji wao kuhusu namna wanavyokabilliana na  changamoto zitokanazo na maradhi ya  ukimwi pamoja na utoaji wa huduma za afya.
 Balozi Manongi akiwa na Professa Estwick ambaye chuo chake kinauhusiano na  ushirikiano na  hospitali ya  Nyakahanga, uhusiano huo  unaokaribia miaka kumi na tatu sasa unahusisha utoaji wa misaada mbalimbali ikiwamo ya vifaa vya hospitali, usomeshaji wa watoto yatima na ujenzi wa Chuo cha Uuguzi ( Nursing Collage) kulia kwa Balozi ni  Bi. Williams ambaye ni mwanafunzi kutoka chuo hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Chuo cha Wauguzi kitasaidia sana kupata wauguzi waliosomea fani hiyo na hivyo kuboresha huduma ya Afya Karagwe.

    ReplyDelete
  2. Tunahitaji wadau wengi kama hawa. Wasinde Karagwe wapelekeni hata Sumbawamga. Juhudi nzuri sana.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...