WATU saba wakiwemo wafanyakazi wawili wanawake wa benki ya  Barclays wamepandishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la kula njama na unyang'anyi wa kutumia silaha pamoja na wiza wa sh milioni 390.2 , dola za kimarekani 55,000 na Euro 2150.

Washtakiwa hao ni Alune Kasililika (38), Neema Batchu (26) wafanyakazi wa benk hiyo, Kakame Julius (38), Iddy Khamis (32), Sezary Msolopa (31), Boniphace Muumba (29) na Ruth Macha (30) wafanyabiashara.

Wakisomewa mashitaka yao mbele ya  hakimu Mkazi, Nyigulila Mwaseba ambapo Wakili wa Serikali Tumaini kweka akisaidiana Mwanaamina  Kombakono  walidai kuwa wastuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili.

Aliieleza mahakama kuwa katika tarehe  tofauti zisizo fahamika washtakiwa  wakiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam walikula njama  kwa nia ya kutenda kosa la wizi.

Katika shtaka la pili washtakiwa wanadaiwa kuwa Aprili 15 mwaka huu, wakiwa katika benki hiyo tawi la Kinondoni, Dar es Salaam waliiba fedha tasilimu sh.
milioni 390.2, Dola za Marekani 55, 000 na Euro 2150 mali ya Barclays.

Hata hivyo, ilidaiwa kuwa kabla ya kufanya wizi huo walimtishia kwa silaha Anifah Ahmad na Anna Tegete ambao ni wafanyakazi wa benki hiyo ili kuweza
kujipatia na kumiliki fedha hizo.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo walikana kuhiska na tukio hilo, ambapo wakili Kweka alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika
wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Mwaseba alisema kwa mujibu wa sheria shtaka la pili halina dhamana, kwa hiyo washtakiwa watakuwa chini ya ulinzi na kupelekwa gerezani hadi Mei 15 kesi hiyo itakapotajwa.
mwaka huu.

Katika tukio hilo ilielezwa kuwa majambazi hao walifika katika benki hiyo Aprili 15, mwaka huu, saa 9:00 mchana wakiwa na magari mawili na bunduki aina ya SMG pamoja na bastola, kisha waliingia ndani ya benki hiyo na kupora fedha walizotoka nazo kwenye mfuko na kukimbia nazo kwa kutumia pikipiki.

Hivi karibuni Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova akizungumza tukio hilo alisema kuwa wamegundua baadhi ya matukio ya wizi wa fedha unafanywa na wafanyakazi wa benki.


Alisema katika wizi huo, robo tatu ya fedha zote zilizoibwa zilichukuliwa siku moja kabla ya tukio linalodaiwa kutengenezwa la wizi, kwa lengo la kuficha wizi huo na kwamba kulikuwa na vikao mbalimbali vya maandalizi ya kufanikisha tukio hilo.

Alisema Aprili 15, mwaka huu siku ambayo wizi huo unatajwa kufanyika, kilichotokea ni tukio la kukamilisha njama hizo.

“Tukio hili lilileta utata tangu mwanzo tulipokwenda kukagua eneo la tukio, kwani siku moja kabla, yaani Aprili 14, gari la kubebea fedha kupeleka Benki Kuu lilifika katika tawi hilo kama ilivyo kawaida lakini fedha hazikutolewa kumbe ilikuwa ni mkakati uliowekwa kufanikisha wizi huo.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 03, 2014

    Meneja mmoja wa Benki ya taifa wa siku nyingi alisema baadhi ya vijana wanaoajiriwa benki zetu sasa wanataka baada ya muda kidogo wa kuanza kazi wawe wameshanunua gari baada ya mwaka wawe na harusi ya kukata na shoka baada ya miaka miwili wawe wameshajenga nyumba. Ingekuwa wanafanya hivyo kwa mikopo halali isingekuwa shida ila wengi wanatafuta njia za mkato na dili ofisini. Tujifunze vijana maisha hayaendi hivyo msijiweke kwenye pressure za bure.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...