· Pampu yadaiwa kupelekwa Morogoro, yeye asema iko kijijini
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa
Maji wa Wilaya ya Chato, Bw. Peter Ngunura kwa kosa la kumdanganya mbele
za watu na kumpa taarifa za uongo juu ya pampu ya maji iliyodaiwa
kupelekwa Morogoro.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Machi
16, 2016) alipokuwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Chato
waliojitokeza kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
uwanja wa michezo wilayani Chato, mkoani Geita.
Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Geita kwa ziara ya siku
mbili akitokea mkoani Kagera, alisimamishwa na wakazi wa kijiji cha
Kalebezo, kata ya Nyamirembe, wilayani Chato na kukuta mabango
yaliyokuwa yakidai maji safi na kuelezea uharibifu wa pampu ya maji.
Katika maelezo yao, wakazi hao walimweleza Waziri Mkuu
kwamba mradi wa maji kwenye kata hiyo ulishakamilika lakini pampu yao
imechukuliwa na kupelekwa Morogoro jambo lililosababisha wakose maji kwa
muda mrefu.
Kwa sababu alikuwa hajafika Chato mjini na hakuwa na
taarifa sahihi za mradi huo wa maji, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao
kwamba analibeba jambo hilo na atafuatilia hadi aelezwe ni kwa nini
pampu hiyo imepelekwa Morogoro. Akiwa kwenye mkutano wa hadhara, ndipo suala la maji likaibuka tena na Waziri Mkuu kuamua kuchukua hatua hiyo.
“It’s unethical (ni kinyume cha maadili) kumdanganya
kiongozi wako. Nimekuuliza mara mbili mbili kama una uhakika kuwa pampu
hiyo ipo ukasema una uhakika kuwa ipo. Nimemtuma diwani na vijana wangu
wakacheki wakasema hakuna pampu,” alisema Waziri Mkuu na kumwita Diwani
huyo jukwaani ili atoe majibu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...