Mwakilishi Mkuu wa Shirika la JICA Tanzania Bwana Toshio Nagase akiongozana na
ujumbe wake amekutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora akiwa
ofisini kwake kueleza nia ya Shirika lake na nchi ya Japan ya kuwekeza kwenye Sekta
ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania.
Bwana Toshio Nagase ameyaeleza hayo akisema kuwa ni muendelezo wa ushirikiano
wa Tanzania na Japan kama ilivyo kwenye sekta nyingine kama vile ya ujenzi na
uchukuzi. Nchi yake iko tayari kuwekeza Tanzania kwa kushirikiana kwa pamoja
kuendeleza Sekta ya Mawsiliano na TEHAMA nchini kupitia ushirikiano wa Serikali ya
Tanzania na Japan; au kampuni na sekta binafsi za Tanzania na Japan.
Bwana Nagase alisema kuwa Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya simu za
mkononi na huduma za mawasiliano ikiwemo huduma za kutuma na kupokea pesa
kupitia kampuni za simu za mkononi.
Hivyo nchi yake ya Japan iko tayari kuendeleza
hilo kwa kuwawezesha watanzania kupata huduma nyingine kama vile bima ya afya
kwa kupitia simu ya mkononi. “Sisi nyumbani mwananchi akipiga simu anapatiwa pointi
ambazo zinamuwezesha kugharamia huduma ya bima ya afya. Jambo hili ni muhimu
kwa wananchi wa Tanzania kupata huduma mbalimbali kupitia simu za mkononi”
alisema Bwana Nagase.
Prof. Faustin Kamuzora alisema kuwa Tanzania imekuwa ni nchi ya kuigwa duniani na
kupigiwa mfano kwa kuwawezesha wananchi kupata huduma ya kutuma na kupokea
pesa kupitia simu za mkononi na kufanya malipo mbalimbali.
Prof. Kamuzora aliongeza
kuwa, “sisi kama Serikali tunawakaribisha wenzetu wa Japan kuja Tanzania kushirikiana
nasi kuendeleza Sekta ya Mawasiliano na kuwekeza nchini kwetu ili wananchi wetu
wanufaike na maendeleo ya Sekta hii kama ambavyo wenzetu wamepiga hatua kwa
kuwa na kampuni za vifaa vya TEHAMA kama vile kampuni ya Sony”.
Kwa upande kwa Sekta ya Mawasiliano Prof. Kamuzora alisema kuwa Wizara iko tayari
kuanzisha viwanda vya TEHAMA vya kutengeneza bidhaa na vifaa vya TEHAMA hapa
nchini kwa ajili ya wananchi na kubuni programu mbalimbali za kompyuta ambazo
zitarahisha na kutatua changamoto za wananchi kuendana na mazingira yetu ya
Tanzania.
Prof. Kamuzora aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali
inayotoa kipaumbele kwenye masuala ya ujenzi na uendeshaji wa viwanda hapa nchini
hivyo Sekta ya Mawasiliano ina nchango mkubwa wa kuiwezesha sekta binafsi na
wawekezaji kuendeleza Sekta ya Mawasiliano hivyo kuongeza fursa ya ajira kwa vijana.
Bwana Nagase amesema kuwa JICA iko tayari kushirikiana na Wizara kuwakutanisha
wafanyabiashara; wawekezaji; kampuni; sekta binafsi na wadau mbalimbali wa Sekta
ya Mawasiliano wa Tanzania na Japan ili kubadilishana uzoefu na kuainisha fursa na
maeneo ya kushirikiana kwa lengo la kuendeleza sekta hiyo na ushirikiano wa nchi hizo
mbili kwenye Nyanja ya TEHAMA.
Aidha, Prof. Kamuzora na mgeni wake Bwana Nagase wamekubaliana kuainisha
maeneo ya kipaumbele ambayo yatafanyiwa kazi kwa pamoja ili kufanikisha uwekezaji
kwenye maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo na ujuzi watanzania;
kuendeleza vijana wenye kampuni zinazohusika na masuala ya ubunifu kwenye
TEHAMA na kuwekeza pia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...