Ni kwa Mafunzo ya Uongezaji Thamani Madini kwa Wanawake
Teresia Mhagama, Arusha

Mkuu wa  Wilaya  ya  Arusha,  Fadhili Nkurlu ameipongeza Kamati ya Maandalizi ya Maonesho ya  Kimataifa ya Madini ya Vito, Arusha kwa  kutoa ufadhili wa mafunzo ya Ukataji na Ung’arishaji  wa madini ya vito kwa wanawake  29 kupitia Mfuko wa Kuwaendeleza Wanawake katika Tasnia ya Madini ya Vito.

Nkurlu alitoa pongezi hizo wakati akifungua  maonesho ya Tano ya  Kimataifa ya  Madini ya Vito, yaliyoanza tarehe 19- 21 jijini Arusha na kuhudhuriwa na takriban washiriki 900 kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka wadau katika sekta ya madini  ya vito kuwaajiri wanafunzi hao pindi wanapohitimu mafunzo yao na kuongeza kuwa, desturi ya kuchangia katika kuendeleza sekta ya madini ya vito ni jambo ambalo linahitaji kuendelezwa na wadau wote ili kuweza kuendeleza sekta hiyo.

Alisema kuwa, Serikali kupitia Kituo cha Jemolojia Tanzania inaendelea kuboresha mafunzo hayo yanayotolewa katika kituo hicho kwa kuanzisha kozi mpya za lapidary  machine na kuongeza kuwa, kabla ya wanafunzi 18 wanaosoma sasa kituoni hapo kuhitimu, watapata mafunzo ya vitendo katika viwanda mbalimbali vinavyoongeza thamani katika madini ya vito.

Aliongeza kuwa, Wizara  ya Nishati na Madini inaendelea kukiboresha Kituo hicho cha Jemolojia kwa kuanzisha kozi za Jemolojia, usonara na hivi sasa iko katika hatua za mwisho za kukamilisha ununuzi wa vifaa  ili viweze kutumiwa katika kozi  zinayotarajiwa kuanza mwezi Septemba mwaka huu.

Alisema kuwa, hizo ni miongoni mwa jitihada zinazofanywa na  Serikali ili kutekeleza Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 ambazo kwa pamoja zinahamasihsa shughuli za uongezaji thamani madini hapahapa nchini ili kuongeza kipato, ajira kwa watanzania na hivyo kukuza uchumi wa nchi.

Mfuko wa kuwaendeleza wanawake katika tasnia ya Ukataji na Ung’arishaji wa madini ya vito ulianzishwa mwaka 2012 na Kamati ya Maandalizi ya Maonesho ya Vito ambayo ilianzisha harambee ya kuwawezesha wanawake kupata mafunzo hayo ya Uongezaji thamani madini.

Darasa la Awamu ya kwanza la mafunzo hayo lilianza Novemba 10, 2014 ambapo wanawake wa kitanzania 15  walihitimu mafunzo husika.Vilevile  Darasa la Awamu ya Pili la mafunzo ya uongezaji thamani madini lilianza Agosti 3, 2015 ambapo wanafunzi 14 walihitimu ambapo darasa linaloendelea kwa sasa lina wanafunzi 18.

Ufadhili wa masomo kwa wanafunzi hao wanawake unajumuisha fedha za chakula, kujikimu, nauli, ada ya miezi Sita, matumizi ya vifaa vinavyohitajika wakati wa mafunzo hayo na malighafi zinazohitajika kwa ajili ya mafunzo husika. 

Viongozi wa Kamati ya Maonesho ya Vito Arusha ni Peter Pereira ambaye ni Mwenyekiti na Katibu wa Kamati ni Elias Kayandabila ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...