MKE wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa amefanya ziara katika Hospitali ya wilaya
ya Ruangwa mkoani Lindi na kutoa msaada wa mashuka kwa akinamama
waliojifungua.
Pia ametumia fursa hiyo kuwapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya
wilaya ya Ruangwa kutokana na kuwahudumia vizuri wananchi na kuwaomba
waendelee kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa maadili ya kazi yao.
Mke wa Waziri Mkuu ameyasema hayo jana wakati alipotembelea wodi ya
akinamama waliotoka kujifungua na kufurahishwa na hali ya utoaji huduma
hospitalini hapo, ambapo aliwasisitiza kuendelea moyo huo kwa sababu wao ndio
wamebeba dhamana ya afya za wananchi.
“Nimefurahi kukuta wazazi wanahudumiwa vizuri na wenyewe wamekiri kwamba
huduma zinazotolewa hospitalini hapa ni za kuridhisha, tofauti na tulivyozoea
kusikia wagonjwa wakiwalalamikia wauguzi, hivyo ni jambo la kujivunia,
hongereni sana” amesema.
Mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika wodi hiyo Hamisa Rashid ambaye
amelazwa katika wodi hiyo amesema alifikishwa hospitalini hapo wiki mbili
zilizopita akiwa katika hali mbaya na ameweza kuhudumiwa vizuri na sasa
anakaribia kutoka.
“Mimi nilikuwa sijitambui, siwezi kufanya kitu chochote lakini baada ya kuletwa
hospitalini hapa madaktari kwa kushirikiana na wauguzi wamenihudumia vizuri na
sasa naweza hata kwenda chooni mwenyewe na bila msaada wao mimi ningekuwa
nimepoteza maisha kutokana na hali yangu ilivyokuwa,” amesema Hamisa.
Mbali na kutoa msaada huo wa mashuka pia ametoa baiskeli mbili kwa ajili ya
wanawake wawili walemavu lengo likiwa ni kuwawezesha kufanya shughuli zao
za kijamii kwa urahisi.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Rehema Omary amemshukuru mke
wa Waziri Mkuu kwa msaada huo, ambapo alimuomba Waziri Mkuu, Majaliwa
awawezeshe kwenda kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na
walemavu ikiwemo michezo.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amewataka
watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuachana na utendaji kazi
wa mazoea kwa sababu umepitwa na wakati.
Pia amesema amefurahishwa na kitendo cha wagonjwa kukiri kuwa
wanahudumiwa vizuri tofauti na hospitali zingine hivyo kuwataka kuendelea na ari
hiyo ya kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi mkubwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...