TIMU ya soka ya Uchukuzi Sports Club mwishoni mwa wiki ilitoka sare ya kufungana bao 1-1
na Amadori Boys ya Pugu Sekondari katika mchezo wa kirafiki uliofanyika jirani na Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Uchukuzi Sports Club inajiandaa kwa mashindano ya Mei Mosi yatakayoanza Aprili 16 mkoani
Dodoma, ambapo mechi hiyo ni ya pili ya majaribio baada ya ile ya kwanza iliyofanyika hivi
karibuni.
Katika mchezo huo, Uchukuzi SC ndio walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Isack
Ibrahim katika dakika ya saba kabla ya Christian Moyo hajasawazisha mwanzoni mwa kipindi
cha pili.
Hatahivyo, Ibrahim alikosa magoli kadhaa ya wazi, baada ya walinzi wa Amadory Boys
kumkaba baada ya kuona ni tishio langoni mwao.
Meneja wa Uchukuzi SC, Robert Damian aliyewahi kuichezea Simba ya Jijini Dar es Salaam,
alisema kuwa mechi hizo za kirafiki zinawasaidia makocha wa timu yao kujua makosa ya
wachezaji wao na kuyarekebisha kabla ya kwenda kwenye kituo cha mashindano, ili waweze
kufanya vizuri.
Alitamba kuwa timu yao ya soka pamoja na nyingine za netiboli, kuvuta kamba, riadha, bao,
drafti na vishale zitafanya vizuri katika mashindano hayo ya Mei Mosi kwani zimejiandaa vizuri,
kwa kupata mechi kadhaa za kirafiki.
Aidha, timu ya netiboli ya Uchukuzi SC juzi ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Bandari
Kurasini huku ikiwa na wachezaji wake wakongwe kama akina Matalena Mhagama, Subira
Jumanne, Fanuna na wengineo, ambao wanaipa nguvu timu hiyo chini ya kocha wao mzoefu
Judith Ilunda.
Timu ya Uchukuzi SC katika mashindano yaliyopita ya Mei Mosi yaliyofanyika jijini Mwanza,
iliweza kutwaa makombe 13, kati ya hayo matano ni ya ubingwa katika michezo ya kuvuta
kamba, baiskeli, bao, karata na riadha kwa upande wa wanawake na wanaume, wakati
yaliyosalia ilishika nafasi ya pili na tatu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...