Na Catherine Sungura, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuzindua huduma zote Za kiuchunguzi za magonjwa kwenye hospitali ya kisasa ya Benjamin Mkapa iliyopo mjini Dodoma
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati alipotembelea hospitali hiyo na kuona inavyoendelea kutoa huduma za afya kwa wananchi
Waziri Ummy alisema serikali imejipanga katika kutekeleza ahadi yake kwa wananchi katika utoaji huduma bora na za kisasa katika hospitali hiyo
"Nawaahidi nitafanya uzinduzi rasmi wa huduma za uchunguzi wa magonjwa ili wananchi waelewe hospitali yetu inatoa huduma zipi ili kila mwananchi atambue nini kinapatikana hapa"alisema Mhe.Ummy
Aidha,Waziri Ummy alisema licha ya kazi nzuri inayofanywa na watoa huduma wa afya wa hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuahidi kuwasiliana na wizara ya Nishati na Madini ili kutatua tatizo hilo.
Hata hivyo alisema wizara yake inafuatilia upatikanaji wa fedha kiasi cha shilingi milioni 137 za kukamilisha ujenzi wa ufungaji wa baadhi ya vifaa tiba vilivyopo hospitalini hapo na hivyo kuwakaribisha wananchi wote kufika hospitali hapo kupata huduma za kibingwa za ugonjwa wa kisukari
Mhe Ummy amesisitiza kuanza kutolewa kwa huduma za vipimo (kama MRI na CT Scan) katika Hospitali hiyo ili kuwapunguzia kero wananchi wa mikoa ya kanda ya kati kupata huduma hizo Dodoma badala ya kusafiri hadi Dar es salaam kupata huduma hizo.
Hospitali ya Benjamin Mkapa ipo katika chuo kikuu cha Dodoma,kwa sasa inahudumia wagonjwa zaidi ya 170 kwa siku,ikikamilika itakua inafanya uchunguzi wa magonjwa ya figo,kisukari pamoja na moyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (katikati) akitembea kukagua majengo ya hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Mjini Dodoma,kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali Hiyo Profesa Ainory Gessase.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Profesa Ainory Gessase (mwenye koti jeupe) akimfafanulia jambo waziri wa Afya wakati alipotembelea hospitalini hapo na kujionea jinsi wanavyotoa huduma kwa wananchi.
Waziri Ummy Mwalimu akikagua baadhi ya vifaa tiba vilivyopo kwenye hospitali hiyo ambapo zinahitajika shilingi milioni 137 za kitanzania kuweza kufunga vifaa vya kiuchunguzi vya magonjwa ya moyo na figo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...