Na Dac Popos, Globu ya Jamii.
Kama inavyofahamika kuwa kila mashindano huwa na kanuni zinazosimamia mashindano husika, sasa basi kuelekea mashindano haya ya Copa Amerika waandaaji wamefanya marekebisho ya kanuni mbili ambazo zimetumika na kuzoeleka katika mashindano mbali mbali ikiwemo haya ya Copa Amerika. Kanuni zilizofanyiwa marekebisho ni kanuni ya 'MUDA WA NYONGEZA' na ile ya 'KADI YA NJANO'.
Kanuni ya muda wa nyongeza (EXTRA TIME) ambayo katika mashindano haya kwa miaka yote imekuwa ikitumika kuanzia ngazi ya mtoano, robo fainali, nusu fainali na fainali iwapo timu zinatoka sare katika muda wa kawaida wa dakika 90, basi huongezwa dakika 30 na mshindi asipopatikana hupigwa mikwaju ya penati tano tano na mshindi kupatikana, kwenye michuano hii sheria hii itatumika katika mchezo wa FAINALI pekee. Kwenye hatua nyingine haitatumika bali timu zikienda sare basi moja kwa moja zitapigiana penati.
Sababu zilizotolewa na waandaaji wa mashindano zinasema kuwa kwa hivi sasa nchini Marekani hali ya hewa ni joto kali sana. hivyo wachezaji wakicheza kwa dakika 120 yaani dakika 90 za kawaida na dakika 30 za nyongeza basi watakuwa wamechoka sana hali inayopelekea kushindwa kupiga penati kwa uzuri zaidi.
Nayo kanuni ya kadi ya njano (YELLOW CARD) ambayo hutumika kwa mchezaji yoyote anayepata kadi tatu za njano basi hukosa mechi mbili zinazofuatia, katika mashindano haya ni kuwa mchezaji akipata kadi mbili za njano basi atakosa mchezo mmoja unaofuata.
Lakini rekebisho lingine hapo hapo kwenye kadi ya njano ni kuwa mchezaji iwapo atapata kadi mbili kabla ya mchezo wa FAINALI yaani kwenye mchezo wa robo na nusu fainali, kadi hizo zitafutwa na ataweza kushiriki kwenye kipute hicho cha FAINALI, isipokuwa mchezaji yoyote akipata kadi nyekundu (RED CARD) kwenye mchezo wa nusu fainali hii haitafutwa hivyo ataukosa mtanange huo wa FAINALI.
Hizo ni kanuni mbili zilizofanyiwa marekebisho tunazopaswa kuzifahamu, hebu sasa tuangalie kwa ufupi wasifu wa timu japo mbili zitakazoshiriki kwenye michuano hii.
JAMAIKA
Timu hii ya Jamaica almaarufu kama 'REGGAE BOYS' inatokea kwenye CONCACAF ikishiriki kama waalikwa. Kikosi hiki chenye nyota kama golikipa Andre Blake anayedakia klabu ya Philadephia Union ya Marekani, mlinzi Wes Morgan anayekipiga kwa mabingwa wa EPL Leicester City na Giles Barnes kiungo mahili wa klabu ya Houston Dynamo ya Marekani, chini ya kocha W. Schafer watategemewa kuleta upinzani mkubwa wakitumia mfumo wao wa 4-3-3, wakiwa na nguvu huku wakishambulia kwa kasi.
MAREKANI
Waandaaji wa mashindano haya maalum, pia wana uzoefu na michuano hii kwani wamekuwa wakialikwa mara kwa mara kushiriki kwenye michuani hii. Timu hii itaingia ikiwakosa nyota kadhaa akiwemo Jozy Altidore. Marekani haikuwa na kiwango kizuri msimu uliopita hali inayomfanya kocha Juergen Krinsman kutaka kuirudisha timu kwenye mstari angalau hata wafikie katika nusu fainali ya michuano hii. Marekani ina timu yenye mchanganyiko wa wachezaji wenye umri mkubwa takribani miaka 30 wapatao 8 watachanganyika na vijana wadogo waliochini ya miaka 24 ambao ni hatari sana. Timu hii itawategemea zaidi wachezaji kama Christian Pulsic kinda wa miaka 17 anayekipiga Borussia Dortmund, Kyle Berkerman wa Real Salt Lake ya Marekani, Jermaine Jones wa Colorado Rapids ya Marekani, mlinzi Geoff Cameron wa Stoke City na mshambuliaji Clint Dempsey wa Seattle Sounders FC ya Marekan.
ENDELEA KUTEMBELEA LIBENEKE LA GLOBU YA JAMII KWA TAARIFA ZAIDI ZA MICHUANO HII.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...