Dar
es Salaam
WAKALA ya Mkemia Mkuu
wa Serikali imekusudia kuendesha kampeni maalum ya kupima matumizi ya vilevi kwa
madereva wanaosafirisha abiria na mizigo ikiwa ni hatua ya kukabiliana na
tatizo la ajali za barabarani nchini.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele alipokuwa
akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wadau wa kemikali juu ya matumizi salama ya
kemikali nchini.
Prof. Manyele alisema
utaratibu wa kuwapima madereva hao utaanza hivi karibuni na utawezesha kupunguza
tatizo la ajali barabarani na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutoa
ushirikiano katika zoezi hilo.
“Madereva wote wanaosafirisha
mizigo na abiria watatakiwa kupita
kwenye kipimo ambacho kitaonyesha kama madereva hao wanatumia vilevi, hali hiyo
itasaidia kutatua tatizo la ajali za barabarani nchini”, amesema Prof. Manyele.
Aidha, Prof Manyele
alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kutoa uwezo na uelewa kwa wahusika hasa wasimamizi wa shughuli za kemikali na
matumizi salama juu ya kukabiliana na matukio au ajali za kemikali pale
yanapotokea.
Aliongeza kuwa
mafunzo hayo yamekuja kufuatia uelewa mdogo wa elimu kwa baadhi ya wadau
wanaojishughulisha na masuala ya kemikali kuhusu uzalishaji, uhifadhi,
usimamizi na usafirishaji wa matumizi ya kemikali nchini.
Mbali na hayo, Prof
Manyele alisema kumekuwa na ajali na matukio yanayotokana na kemikali ikiwemo
ya ajali halisi na mengine kutokana na kukosa uelewa wa matumizi sahihi na
salama ya kemikali.
Akifafanua zaidi
Prof. Manyele alisema katika kukabiliana na madhara yatokanayo na matumizi
yasiyo salama ya kemikali, Serikali ilitunga sheria ya Kemikali za Viwandani na
majumbani mwaka 2003 kwa lengo la kuhakikisha kemikali hizo zinatumika katika
hali iliyo salama.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...