Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Mbegu za Mimea kutoka Tanzania hivi
karibuni amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mbegu CAJ ya Shirika
la Kimataifa la Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea Hakilimiki
la Kimataifa (The International Union for
the Protection of New varieties of Plants - UPOV)
Wanachama wa Shirika la Kimataifa la Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya
za Mbegu za Mimea (UPOV) mwishoni mwa mwezi Oktoba walikutana Jijini Geneva,
Uswisi ambapo pamoja na ajenda zingine, walilifanya uchaguzi wa viongozi wa
Shirika hili akiwemo Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na
Utawala (Legal and Administrative
Committee - CAJ). Hii ndiyo Kamati ya juu inayolishauri Baraza la UPOV
kuhusu masuala yote ya kitaalamu na kisheria. Kwa kawaida pamoja na kazi ya
kumsaidia Mwenyekiti wake, Makamu Mwenyekiti huandaliwa kuwa Mwenyekiti mara tu
kipindi cha Mwenyekiti wa CAJ kinapoisha.
Katika uchaguzi huo, Mwakilishi wa
Tanzania kwenye Baraza la UPOV, Bwana Patrick Ngwediagi, alichaguliwa kuwa
Makamu wa Mwenyekiti wa CAJ.
Bwana Ngwediagi ni Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za
Mbegu za Mimea (Tanzania Bara) na anao utaalamu na zoefu mkubwa katika masuala
ya hakimiliki za mbegu, mfumo wa hakimiliki wa shirika la UPOV na tasnia ya
mbegu kwa ujumla na pia ni mkufunzi wa wakufunzi (trainer of trainers) katika
masuala ya hakimiliki za wagunduzi wa mbegu mpya kwa mujibu wa Mkataba wa UPOV
wa mwaka 1991.
Aidha, Bwana Ngwediagi alisimamia na kuratibu kwa weledi mkubwa mchakato
mrefu wa kuiwezesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwanachama wa UPOV.
Mchakato huo ulihusisha kupitishwa kwa Azimio la Bunge kuhusu kuridhia Mkataba
wa UPOV wa mwaka 1991 na kutungwa kwa sheria ya Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina
Mpya za Mbegu za Mimea kwa upande wa Tanzania Bara (2012) na Zanzibar (2014).
Kuanzia tarehe 22 Novemba, 2015, Tanzania ni mwanachama wa 74 wa UPOV na kabla
ya hapo ilikuwa Mwanachama Mwangalizi (Observer).
Bwana Ngwediagi pia ni mbobezi wa masuala ya mbegu katika ngazi ya
Kikanda na Kimataifa. Kwa sasa yeye ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya
Mbegu ya Afrika iitwayo, AfricaSeeds.
Taasisi hiyo inaundwa na nchi wanachama (Inter-governmental
organization) wa Umoja wa Afrika (AU). Africa Seeds ndiyo taasisi iliyopewa
jukumu la kutekeleza na kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Africa Seed and Biotechnology Programme (ASBP) wa Umoja wa Afrika
(AU).
Kuchaguliwa kwa Bwana Ngwediagi
kuwa Makamu Mwenyekiti wa CAJ, pamoja na kuongeza heshima ya Tanzania
kimataifa, nafasi hiyo pia itaitangaza Tanzania na hivyo kuongeza uwekezaji
katika ugunduzi wa mbegu mpya, uzalishaji wa mbegu na kilimo kwa ujumla.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...