Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa Ubalozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China uliopo Zanzibar kwa maandalizi mazuri iliyofanya kuratibu ratiba ya ziara yake ya Siku Tano aliyoifanya hivi karibuni Nchini China.

Alisema ziara hiyo ya Kiserikali ilimuwezesha na kumpa fursa ya kukutana na Uongozi wa Kampuni na Taasisi mbali mbali za China zilizoonyesha nia ya kutaka kuwekeza vitega uchumi vyao Visiwani Zanzibar.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Bwana Xie Xiaolon akimshukuru kwa kukamilisha ziara hiyo kwa mafanikio makubwa.

Alisema Mikutano ya pamoja kati ya Ujumbe wa Zanzibar na Uongozi na Makampuni mbali mbali waliyokutana nayo yalikuwa na muelekeo mwema wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

“ Ratiba yote iliyopangwa ndani ya ziara hiyo imetekelezwa kwa asilimia kubwa na kuonyesha matumaini mapya ya ushirikiano na uhusiano uliopo kati ya China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar kwamba Makampuni ya Umeme ya TBEA, Uvuvi ya Hongdong, ile inayotoa huduma za Kijamii ya Avic pamoja na Kampuni ya MCC – Oversease tayari wataalamu wake wameshaangalia mazingira ya Zanzibar na kujiandaa namna ya kuanzisha miradi yao Zanzibar.

Naye Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Xiaolon alisema Zanzibar na China daima zitaendelea kushirikiana katika njia ya uanzishwaji wa miradi ya pamoja itakayosaidia kuleta ustawi wa wananchi wa sehemu hizo mbili.

Bwana Xie alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuona miradi ya maendeleo iliyoanzishwa kupitia msaada au udhamini wa Serikali ya China itatekelezwa na kukamilika kama ilivyokusidiwa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaolon Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.Mazungumzo hayo yalikuwa na lengo la kuushukuru Ubalozi wa Ubalozi huo kwa kufanikisha uratibu wa Ziara ya Kiserikali ya Balozi Seif aliyoifanya hivi karibuni Nchini China.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...