Frank Mvungi- MAELEZO
Watanzania wameaswa kupunguza unywaji wa pombe ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda na kulifikisha taifa kwenye uchumi wa kati ifikapo 2020.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Prof. Ayoub Maghimba amesema kuwa ni vyema watu wakapunguza unywaji wa Pombe ili kutumia muda mwingi katika uzalishaji na kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na Saratani,magonjwa ya moyo,magonjwa sugu ya njia ya hewa,seli mundu,magonjwa ya akili na dawa za kulevya,magonjwa ya figo,kisukari,ajali, na magonjwa ya macho yasiyo ya kuambukiza” Alisisitiza Prof. Maghimba.
Akifafanua Prof. Maghimba alisema kuwa utafiti uliofanyika ulionyesha asilimia 15.9 ya wananchi wanavuta sigara, asilimia 29.3 wanakunywa pombe, asilimia 97.2 wanakula mbogamboga na matunda chini ya mara tano kwa siku hali inayowaweka katika hatari ya kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Alisema kuwa unywaji wa pombe uliokithiri unasababisha magonjwa kama saratani ambayo inachangia vifo na wastani wa wagonjwa 109 hugundulika na saratani kila siku hapa nchini.
“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza au magonjwa sugu ni magonjwa ambayo mtu akiyapata hawezi kuambukiza wengine na ataishi nayo hadi siku ya kufa.” Alisisitiza Prof.Maghimba.
Magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka duniani kote, hasa kwenye nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara,Tanzania ikiwemo. Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanachangia asilimia 27 ya vifo vyote duniani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...