Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Ujumbe wake wamewasili nchini Zambia kwa ajili ya kufanya ziara ya kutembelea njia nzima ya Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi  la TAZAMA ili kukagua miundombinu yake pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa vituo vinavyotumika kusukuma mafuta hayo.

Ziara hiyo ya kutembelea Mkuza wa Bomba inaanza rasmi leo Tarehe 27 Januari huko Ndola nchini Zambia na kumalizika Tarehe 31 Januari, 2017 Jijini Dar es Salaam..

Ziara hiyo inafuatia makubaliano ya Marais wa nchi husika, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mhe. Edgar Lungu ya Tarehe 28 Novemba, 2016 kuhusu kuboresha Bomba hilo la TAZAMA kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Imeelezwa kuwa Ziara hiyo itafanyika kwa kufuata njia ya Mkuza kwa kupitia vituo vyote vinavyosukuma mafuta na baadaye kikao cha pamoja cha viongozi hao kitakachofanyika jijini Dar es Salaam. 

Ziara hii imechagizwa pia na  ziara ya Rais Lungu  kwenye kituo cha TAZAMA Jijini Dar es Salaam ambapo ilielezwa kuwa ufanisi wa Bomba hilo umeshuka ikilinganishwa na hapo hapo awali kwani lilikuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 1.1 za mafuta kwa mwaka lakini kwa sasa linasafirisha tani 600,000 tu.  

Hivyo ili kuboresha miundombinu ya TAZAMA, nchi hizo zimekubaliana kushughulikia kwa pamoja chanzo cha kuzorota kwa utendaji kazi wa TAZAMA ili Bomba hilo liweze kuendeshwa kwa faida kwa kunufaisha pande zote mbili.

Ziara  hiyo pia imelenga kufanya tathmini kwa kukagua Mkuza wa Bomba na maeneo yanayopendekezwa kujengwa bomba la kusafirisha Mafuta Safi (Finished Product) na Gesi Asilia kutoka Tanzania hadi Zambia kupitia njia ya Mkuza huo (wayleave) wa Bomba la TAZAMA.

Imeelezwa kuwa ziara hiyo itafanywa kwa ushirikiano wa Mawaziri wa Nishati kutoka Tanzania na Zambia wakiambatana na Makatibu wakuu, pamoja na viongozi waandamizi kutoka nchi zote mbili sambamba na uongozi wa TAZAMA.

Bomba la kusafirisha mafuta ghafi la TAZAMA linaloanzia nchini Tanzania hadi mji wa Ndola nchini Zambia lina urefu wa kilomita 1,710 na kipenyo cha inchi 8 hadi 12 na lilianza kazi Mwaka 1968.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza jambo alipowasili katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kenneth Kaunda Jijini Lusaka, Zambia. Kulia ni Balozi wa Tanzania Nchini Zambia, Balozi Grace Mujuma.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kulia) na ujumbe wake kutoka Tanzania walipowasili Lusaka Nchini Zambia. Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania Nchini Zambia, Balozi Grace Mujuma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Zambia, Brigedia Jenerali Emelda Chola na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kutoka Tanzania, Profesa Justin Ntalikwa.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akizungumza jambo alipowasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda Jijini Lusaka, Zambia.  Kulia ni Balozi wa Tanzania Nchini Zambia, Balozi Grace Mujuma na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiongozana na  Balozi wa Tanzania Nchini Zambia, Balozi Grace Mujuma (kulia) alipowasili Jijini Lusaka, Zambia kwa ajili ya ziara ya kutembelea Bomba la TAZAMA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...