Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali imesema itazichukulia hatua Taasisi zote zilizokiuka sheria na kanuni za manunuzi ya Umma pamoja na zile zenye viashiria vya rushwa ambazo zimebainika katika ripoti ya tathmini ya utendaji iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa mwaka wa Fedha 2016/17.
Hayo yamesemwa leo Mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alipokuwa akipokea ripoti ya tathimini ya utendaji wa Taasisi za Serikali katika sekta ya Manunuzi iliyofanywa na PPRA kwa mwaka wa Fedha 2016/17.
“Tutazichukulia hatua na kuziwajibisha taasisi zote ambazo zimebainika katika ripoti hii kuwa na viashiria vya rushwa au kufanya malipo yenye utata katika manunuzi yao,” alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango amesema kuwa, zaidi ya 70% ya fedha za Umma zinatumika kununua vifaa na huduma mbalimbali hivyo Serikali haitavumilia kuona fedha hizo zinatumika bila kufuata sheria na kanuni zilizowekwa
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Balozi Dkt. Matern Lumbanga amesema kuwa kuna taasisi nane zilizofanyiwa uchunguzi maalum kufuatia maelekezo kutoka mamlaka za juu ambazo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Mifupa (MOI) pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Taasisi nyingine ni Shirika la Bima la Taifa (NIC), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Anga (TCAA), Wizara ya Fedha na Mipango na Halmashauri ya Wilaya Kondoa.
Balozi Lumbanga amesema kuwa uchunguzi wa zabuni mbili zenye thamani ya shilingi bilioni 160.5 ambazo zilikuwa zinatekelezwa na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja TCAA haukubainika mapungufu ya msingi na PPRA ilipendekeza utekelezaji wa miradi hiyo uendelee kama ilivyopangwa.
“Uchunguzi uliofanywa katika taasisi sita zilizobaki ulibaini kuwa Serikali ilipata hasara ya takribani shilingi milioni 12.15 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo, ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi uliosababisha ongezeko la riba pamoja na faini zilizotokana na ukiukwaji wa taratibu za kijamii na mazingira kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa kazi za ujenzi,” alisema Balozi Lumbanga.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akionesha kwa wanahabari na wajumbe wengine wa Bodi(hawapo pichani) kitabu cha Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 Leo Mjini Dodoma, , Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) Balozi Dkt. Matern Lumbanga.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiongea na wajumbe wa Bodi ya ya Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) baada ya kupokea Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 Leo Mjini Dodoma ambapo ameahidi kuzichukulia hatua taasisi zote zilizokiuka taratibu za manunuzi zilizoainishwa kwenye Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...