Kumekuwa na taarifa potofu katika mitandao ya kijamii kuwa wafuasi 11 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilayani Ikungi walikamatwa kwa kosa la kuendesha michango kwa ajili ya Mbunge wa Singida Mashariki, Mhe. Tundu Lissu aliyejeruhiwa kwa risasi na watu wasiojulikana. 
Ukweli ni kwamba taarifa hizi ni potofu na zenye lengo la kuwafitinisha wana Ikungi na jimbo la Singida Mashariki kwa ujumla. Viongozi waliokamatwa na ambao baadaye walihojiwa na kuachiwa kwa dhamana hawakuwa wakiratibu michango yoyote bali walikutwa wakiandika mabango yenye uchochezi dhidi ya viongozi wa Serikali na wakitaka kuandamana bila kibali. 
Wakati Mhe Lissu anaendelea kupatiwa matibabu nje ya nchi na Serikali ikiwa inalifuatilia jambo hili kwa karibu ili kuwachukulia hatua kali wote waliohusika, natoa rai kwa wana Ikungi kuwa ni vyema tukaungana badala ya kuingiza siasa na mihemko katika jambo hili kama Taifa lilivyoungana katika tatizo la Kibiti ambalo sasa limemalizika. 
Aidha, kwa kuwa tayari viongozi wa kitaifa wa Chadema wameshatangaza utaratibu wa kuchangia, nawashauri viongozi wa chama hicho wilaya kutumia mkondo huo. Vile vile, kwa wadhifa wangu, nimeshamwagiza Mwenyekiti wa Halmashauri yetu ya Ikungi ili aitishe kikao cha madiwani wote kuweka utaratibu wa pamoja wa namna gani ya kuchangia matibabu ya mbunge wetu. 
Nichukue fursa hii kumpa pole Mhe. Lissu na wananchi wenzangu wa Ikungi na mahsusi jimbo la Singida Mashariki kwa tukio hili baya. Serikali ya Wilaya inalaani vikali wote waliohusika katika tukio hili ambalo linakwenda tofauti na mila na desturi za Kitanzania.  
Tunamwombea Mhe Lissu nafuu ya haraka ili aweze kurejea kwenye majukumu yake ya kuwatumikia wananchi.

Imetolewa na: 
Ndugu Miraji J. Mtaturu 

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...