Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeahidi kutoa timu ya wataalamu watakao suluhisha mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida na Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara.
Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Singida katika kijiji cha Singa tarafa ya Kinampundu Wilayani Mkalama ambapo amesema Wizara yake itatoa wataalamu watakaoweza kutatua mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 30.
“Kwakuwa pande zote mbili za Mkalama na Hanang’ zimekutana mara kadhaa bila mafanikio, nitaleta wataalamu wafike eneo la mpaka ili wataalam hao wawasomee alama moja baada ya nyingine, kila mmoja wenu afahamu eneo lake mwisho ni wapi, nadhani hapo tutakuwa tumewasaidia wananchi wetu”, amesema Dkt Mabula.
Amesema wananchi wa Kijiji hicho cha Singa wasiwe na wasiwasi endapo baada ya kuonyesha mpaka wao mashamba yao yakionekana yapo wilaya ya Hanang’ wataruhusiwa kuendelea kuyamiliki ila watatakiwa kwenda kujitambulisha katika Uongozi wa Wilaya hiyo.
Aidha Dkt Mabula amesema timu hiyo ya wataalamu itahakikisha inasuluhisha migogoro yote ya mipaka ya wilaya hiyo ambayo ngazi ya wilaya imeshindikana kutatuliwa.
Amewashauri wananchi hao kutouza au kugawa ardhi yao ovyo ovyo kwakuwa ardhi ni mali na mtaji popote pale hata kama ni vijijini hivyo watunze ardhi yao na kuiongezea thamani kwa kuipima na kuwa na hati ya umiliki.
Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akizungumza na wataalamu wa ardhi, viongozi na watendaji wa halmashauri ya Wilaya na Manispaa ya Singida [hawapo pichani], Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi.
Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akizungumza na wananchi wa kijiji cha Singa tarafa ya Kinampundu Wilayani Mkalama, Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jaksoni Massaka.
Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Ardhi wa Wilaya ya Iramba Lugano Sanga kuhusu utuzanji wa nyaraka za idara hiyo.
Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi hati ya kumiliki kiwanja chake kilichopo Mjini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...