Wanachama wa Mtandao wa Polisi Wanawake Arusha pamoja na watoto
yatima wa kituo cha Christ Hope Orphonage wakionekana kusikiliza kwa
umakini hotuba iliyokuwa inatolewa na mlezi wa Mtandao huo Kamanda wa
Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo.
Askari wapatao 80 toka wilaya mbalimbali za mkoa wa Arusha ambao
ni wanachama wakitembea kwa maandamano umbali wa kilomita 7 huku
wakiongozwa na Brass Band ya Polisi.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
MTANDAO wa Polisi
Wanawake mkoa wa Arusha umetakiwa upambane kwa kujitoa na kutoa elimu katika
maeneo mbalimbali ya mkoa huu ili kuweza kutokomeza ndoa za utotoni kwa baadhi
ya makabila.
Hayo yameelezwa leo
na mlezi wa mtandao huo mkoani hapa ambaye pia ni Kamanda wa Polisi mkoa wa
Arusha Naibu kamishna (DCP) Charles Mkumbo wakati wa maadhimisho ya miaka kumi
tangu kuanzishwa kwa mtandao huo yaliyolifanyika katika kituo cha kulelea
watoto yatima kiitwacho CHRIST HOPE ORPHANAGE kilichopo Uswahilini halmashauri
ya jiji la Arusha.
Aliwataka wasimame
imara ili kuhakikisha elimu juu ya unyanyasaji na ukatili kwa watoto, akina
mama na akina baba inatolewa na kuwafikia walipo hali ambayo itasaidia kuondoa
kabisa tatizo hilo.
Kamanda Mkumbo alisema
wakati umefika sasa kwa Madawati ya Jinsia na watoto kutokaa ofisini na badala
yake wanatakiwa waifuate jamii ilipo kwani wanaokwenda kutoa taarifa kwenye
vituo vya Polisi ni sehemu ndogo tu ya wengi wenye kukosa elimu ya uelewa juu
ya ukatili na unyanyasaji waliopo mitaani.
“Wale wanaokwenda kutoa
malalamiko yao katika vituo vya Polisi ni wachache sana ukilinganisha na wale
wenye matatizo hayo waliopo mitaani au kwenye taasisi mbalimbali kama vile shule”
Alisema kamanda Mkumbo.
“Watu wengine mpaka
leo hii wanaamini ukeketaji ni moja ya mila yao kitu ambacho sio sahihi hivyo
kupitia madawati ya Jinsia na Watoto pamoja na taasisi nyingine zikishirikiana
na kutembelea jamii kwa nia ya kuwaelimisha naamini kwamba matatizo haya
yataisha”. Aliongeza Kamanda Mkumbo.
Aliwatake wanachama
wa mtandao huo ambao ni Polisi Wanawake kufanya kazi kwa bidii ili kuidhihirishia
jamii kwamba wanaweza bila kuwezeshwa. Alimalizia Kamanda Mkumbo.
Awali akieleza
madhumuni ya maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake mkoa wa Arusha
Mrakibu wa Polisi Namsemba Mwakatobe, alisema
kwamba mtandao huo una wajibu wa kushirikiana na na makundi mbalimbali wakiwemo
watoto yatima hali ambayo itasaidia makundi hayo kutambua kwamba, hawapo peke
yao bali mtandao huo upo nyuma yao katika kusikiliza matatizo yao na kulinda
haki zao.
Alisema pamoja na
kuungana nao siku ya leo lakini pia mtandao huo umejitokeza kwa ajili ya kuonyesha upendo wao kwao kama
askari lakini pia kama wa kike na kuhakikisha kwamba wanakuwa katika mazingira
salama na kuepuka vitendo vya uhalifu.
Akizungumza katika
maadhimisha hayo Mkurugenzi wa kituo hicho Bw. Steven Isanja alisema kituo
hicho kilianzishwa mwaka 2007 kikiwa na watoto 30 lakini hivi sasa kina watoto
64 ambao wanasoma katika ngazi ya Chekechea, Shule ya Msingi na Sekondari.
Maadhimisho hayo yaliyojumuisha
jumla ya askari wanawake 80 kutoka
wilaya za mkoa huu yalianzia katika kituo kikuu cha Polisi Arusha ambapo walitembea
kwa maandamano umbali wa kilomita 7 kisha kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa
watoto wa kituo hicho kama vile Mchele kilo 100, Mbuzi wawili, mafuta lita 40,
sabuni vinywaji mbalimbali vyote vikiwa
na thamani ya Shilingi 780,000/= pamoja na fedha taslimu shilingi 160,000/=.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...