Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ametoa pongezi nyingi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA) kwa kufanikiwa kutoa huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 100 kwa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Hayo aliyasema alipokuwa akizindua Mradi mkubwa wa Maji wa Manga’na, uliopo Kata ya Uru Kaskazini, utakaohudumia zaidi ya vijiji 11 katika Manispaa ya Moshi na Wilaya ya Moshi Vijijini baada ya kupokea taarifa ya hali ya huduma ya maji katika Mji wa Moshi.

“Nawapongeza MUWSA kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya, kwa kuwa ndio lengo la Serikali, kuwa ifikapo mwaka 2020 maeneo ya vijijini huduma ya majisafi na salama ifikie asilimia 85 na mijini asilimia 95. Nyinyi leo hii mmeshavuka lengo hilo kwa Manispaa ya Moshi, kwa kweli nimefurahishwa sana na jambo hili na mnastahili pongezi nyingi’’, alisema Mhandisi Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe aliendelea kusema kuwa kwa kufanikiwa lengo hilo, mamlaka hiyo sasa itaongezewa maeneo mengine zaidi, ili kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wengine wa Moshi Vijijini ambao hawajafikiwa na huduma ya maji, na kuahidi kama Waziri mwenye dhamana ya maji atawatafutia fedha kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tenki la Maji la Njari.


Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira wakifungua bomba kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Maji wa Mang’ana.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amkimtua ndoo kichwani mama kutoka Kijiji cha Mang’ana, akiashiria kutimiza lengo la Serikali ‘‘kumtua mama ndoo kichwani’’ baada ya uzinduzi wa Mradi wa Mang’ana.
Msafara wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ukielekea kwenye Chanzo cha Maji cha Mang’ana katika uzinduzi wa Mradi wa Mang’ana.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...