JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIAKURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amerejea jijini Dar es Salaam jioni tarehe 28 Novemba, 2017 kutoka Mjini Nairobi nchini Kenya ambako amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokelewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Sherehe za kuapishwa kwa Mhe. Uhuru Kenyatta zimefanyika katika uwanja wa Moi Kasarani na kuhudhuriwa na viongozi kutoka nchi mbalimbali wakiwemo Marais, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri na Mabalozi.
Pamoja na kumwapisha Mhe. Uhuru Kenyatta kuwa Rais kwa kipindi cha pili, Jaji Mkuu wa Kenya Mhe. David Maraga amemwapisha Naibu Rais Mhe. William Ruto.
Akizungumza baada ya kuapishwa Mhe. Uhuru Kenyatta ameahidi kuiongoza Kenya bila kubagua, kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chake cha kwanza na kuimarisha zaidi huduma za afya, makazi bora kwa wananchi, kuendeleza viwanda, kuinua kilimo, kukabiliana na ukame na kusimamia vizuri utumishi wa umma.
Aidha, Mhe. Rais Uhuru Kenyatta ameahidi kuimarisha zaidi ushirikiano wa Kenya na nchi za Afrika huku akitilia mkazo ushirikiano wa Afrika Mashariki na ametaka wananchi wa Kenya wawe kitu kimoja na wailinde amani.
Kabla ya kuondoka nchini Kenya, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amemtembelea na kumjulia hali Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu ambaye amelazwa katika hospitali ya Nairobi na kumfikishia salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Mhe. Tundu Lissu amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa salamu zake na kumtuma Makamu wa Rais akamuone hospitalini.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Novemba, 2017
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan akimpongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya kwa awamu ya pili, katika Sherehe zilizofanyika leo kwenye uwanja wa Moi Kasarani Mjini Nairobi, Kenya. Mhe. Samia Suluhu Hassan amehudhulia sherehe hizo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan (wa tatu kulia) akiwa pamoja na viongozi wengine wa nchi mbalimbali waliohudhulia katika Sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Rais Uhuru Kenyatta iliyofanyika leo kwenye uwanja wa Moi Kasarani Mjini Nairobi, Kenya. Mhe. Samia Suluhu Hassan amehudhulia sherehe hizo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. PICHA NA IKULU.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...