Na Mwandishi Wetu
WAHITIMU wa Shule kongwe ya Sekondari Ndanda iliyopo Masasi mkoani
Mtwara, kupitia umoja wao (UWAHISSENDA) wanakusudia kuanzisha kampuni
itakayotoa mikopo midogomidogo kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi.
Hatua hiyo imekuja miaka miwili baada ya wahitimu hao kuanzisha kundi
la mtandao wa kijamii la Whatsaap lenye zaidi ya wanaumoja 250, na
hivyo hivi karibuni kuazimia pamoja na kuimarisha umoja wao, wafikirie
pia kuinuana kiuchumi.
Akizungumza baada ya kikao cha wanaumoja hao hivi karibuni, Kaimu
Mwenyekiti wa UWAHISSENDA, Yohana Kasawala alisema dhamira yao itaanza
kutekelezwa mapema mwakani baada ya kuwa tayari wameshapata mtaji
kutokana na michango ya wanachama.
Alisema, pamoja na kukopeshana huku riba ikitumika kutunisha mfuko wa
umoja, wanakusudia kutanua wigo wa mikopo hata kwa wasio wanaumoja wa
UWAHISSENDA.
Aidha, mipango hiyo ya kuinuana kiuchumi inakwenda sambamba na mpango
wa uzinduzi wa umoja huo uliopangwa kufanyika shuleni Ndanda mapema
mwakani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 90 tangu kuanzishwa
kwa shule hiyo.
“Daima umoja ni nguvu, utengano ni dhaifu, nasi tumeona ni vyema
tukatumia mshikamano huu kama fursa ya kujiimarisha kiuchumi. Tuna
ndoto nyingi, lakini kwa kuanzia tunakuja na hili la kampuni ya mikopo
midogomidogo yaani Microfince company…
“Wataalamu wetu wa uchumi ndani ya umoja ambao wametapakaa katika
taasisi za fedha nchini wametupatia mchanganuo wenye kutia matumaini
kwamba tutaweza, na kama mambo yatakwenda hivyo, siku za usoni
tunaweza kufikiria hata kuanzisha benki…Ni suala la muda tu,” alisema
Kasawala na kuongeza kuwa, umoja una Katiba, umesajiliwa kisheria na
kufuata taratibu nyingine za nchi.
Ndanda, shule iliyoanzishwa mwaka 1928, ni miongoni mwa shule kongwe
zilizotoa wasomi wengi waliobahatika kushika nyadhifa mbalimbali
katika nchi, miongoni mwao
akiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Pia wamo Hawa Ghasia, mmoja wa mawaziri waandamizi katika Serikali ya
Awamu ya Nne chini ya Utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Subira Mgalu,
Naibu Waziri wa Nishati katika Serikali ya Rais, Dk John Magufuli pia
ni matunda ya sekondari ya Ndanda.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...