WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameungana na wanafamilia, wananchi wa Songea katika kuomboleza kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo la Songea, Bw. Leonidas Gama, nyumbani kwa marehemu Likuyu wilayani Songea. 
Marehemu Gama amefariki dunia jana Ijumaa, Novemba 24, 2017 katika Hospitali ya Peramiho mkoani Ruvuma alikokuwa akipatiwa matibabu. Marehemu anatarajiwa kuzikwa Jumatatu, Novemba 27, 2017 katika kijiji cha Likuyu wilayani Songea.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu amesema kifo hicho ni pigo kwa Serikali kwa sababu marehemu alishirikiana nayo vizuri tangu akiwa mtumishi wa umma na hata baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Songea. 
 Waziri Mkuu amesema msiba huo umeleta mtikisiko mkubwa kwa sababu baada ya kurudi nchini kutoka India alikokuwa akipatiwa matibabu aliwaeleza kuwa hali yake kwa sasa ni nzuri. ”Ametuachia pengo kubwa ambalo hatuna namna ya kuliziba.” 
 Ameongeza kuwa alipokea taarifa za msiba huo kwa huzuni na mshtuko mkubwa kwa sababu siku mbili kabla ya Waziri Mkuu kuanza ziara yake mkoani Ruvuma, Bw. Gama alimpigia simu na kumjulisha kwamba yeye anatangulia Songea kumpokea. 
 “Kifo ni mipango ya Mwenyezi Mungu na kwamba Bw. Gama ametangulia nasi tutafuata, hivyo wajibu wetu sote ni kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema. Gama alikuwa kiongozi na mwanga wa maendeleo.” 
 Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaomba wanafamilia, mke wa marehemu na watoto na wananchi wa jimbo la Songea waendelee kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu.” 
 Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bibi Christine Mndeme alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutenga muda wake na kwenda kuwafariji wafiwa licha ya majukumu mengi na makubwa aliyonayo. 
 Awali msemaji wa familia Bw. Issa Fusi alimshukuru Waziri Mkuu pamoja na viomgozi mbalimbali waliojitokeza na kuwafariji baada ya kutokea kwa msiba huo.”Kaka yetu tulimpenda sana kazi ya Mungu haina makosa.”
 Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Songea  Marehemu Leonidas Gama. Waziri Mkuu aliungana na wanafamilia pamoja na wananchi wa Songea katika kijiji cha Lukuyi Wilayani Songea leo Novemba 25/2017 katika kuomboleza msiba huo.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akiongea machache  nyumbani kwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Songea  Marehemu Leonidas Gamaambako aliungana na wanafamilia pamoja na wananchi wa Songea katika kijiji cha Lukuyi Wilayani Songea leo Novemba 25, 2017  kuomboleza msiba huo.
Picha na habari na Ofisi ya Waziri Mkuu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...