Na Hamza Temba - Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii,
Dk. Hamisi Kigwangalla leo Januari 25, 2018 mjini Dodoma ametaja majina ya
watuhumiwa wa ujangili ambao wengi wao ni wamiliki na washirika wa Kampuni za
uwindaji wa kitalii na kuwapa siku saba wawe wamefika kwa hiari yao wenyewe
katika ofisi za Wizara hiyo Mjini Dodoma, Swagaswaga House kwa ajili kutoa
maelezo kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kujibu tuhuma hiyo na nyingine
nyingi zinazowakabili mbele ya kamati atakayoiunda.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Dk. Kigwangalla ametaja baadhi ya tuhuma hizo ambazo ziko kinyume cha sheria na taratibu za uwindaji wa kitalii kuwa ni uwindaji
haramu, uhawilishaji wa umiliki wa vitalu vya uwindaji pasipo kufuata sheria, udanganyifu
kwenye kujaza fomu za uangalizi, rushwa,
uhalifu dhidi ya rasilimali za wanyamapori na uhujumu uchumi.
Alitaja tuhuma zingine kuwa ni
ukiukwaji wa kanuni za uwindaji (kupiga wanyama usiku, kuwinda wanyama bila
kujali umri, kupiga wanyama nje ya maeneo waliyopewa), kukutolipa tozo
mbalimbali za maendeleo za jamii kwenye vijiji jirani na maeneo wanaoendesha
biashara ya uwindaji, kushindwa kuendesha ipasavyo shughuli za kuzuia ujangili.
Dk. Kigwangalla aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni ndugu Pasanis na wenzake ambao wanamiliki kampuni ya Berlette Safari Corporation Ltd na Ngugu Shein Ralgi na wakurugenzi
wenzake wa kampuni ya Game Frontiers of Tanzania Ltd.
Wengine ni Ndugu Howel na wakurugenzi wenzake wa kampuni ya
Mkwawa Hunting Safaris Tanzania Ltd, Ndugu Thomas Fredikin na wenzake wa Kampuni
ya Mwiba Holdings Ltd, Wengert Windrose Safaris Tanzania Ltd na Tanzania Game Trackers Safaris Ltd, na
Ndugu Awadh na wenzake ambao wanamiliki kampuni ya Uwindaji wa Greenmiles
Safaris Ltd.
Aliwataja washirika wengine kuwa ni Ndugu ni Kwizema, Ndugu
Robert, Ndugu Solomon Makulu, Ndugu Siasa Shaban, Ndugu Hamis Abdul Ligagabile na
mtumishi wa Wizara Wizara ya Maliasili na Utalii, Alex Aguma.
Katika hatua nyingine Dk.
Kigwangalla ametoa Ilani ya siku 30 kwa watu mbalimbali ikiwemo Mawaziri Wakuu
Wastaafu waliovamia kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini
Arusha wafike kwa Kamishna Mkuu wa Ardhi waweze kuhakikiwa na kuthibitisha
umiliki wao halali ama sivyo wavirejeshe Serikalini viweze kumilikishwa kwa mmiliki
wake halali.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara hiyo Mjini Dodoma leo. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Aloyce Nzuki.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...