Naibu Waziri wa ujenzi, Elias Kwandikwa, ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kulihamisha bomba la gesi lililopitishwa katika maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Mtwara kabla ya bomba hilo halijaleta madhara kwa watumiaji wa Uwanja huo.
Akizungumza mkoani Mtwara, mara baada ya kukagua uwanja huo, ikiwa ni siku kadhaa baada ya kutokea kwa tukio la ajali ya bomba la gesi katika maeneo ya Buguruni kwa Mnyamani mkoani Dar es salaam na kusababisha madhara kwa wananchi, Naibu Waziri huyo amesema kuwa uwepo wa bomba hilo katika uwanja huo si salama na huenda ikapelekea watoaji huduma za usafiri wa anga kusitisha au kutokuleta kabisa huduma zao kutokana na hofu, hali itakayopelekea Serikali kukosa mapato.
“TAA, TPDC na wataalam wa Wizara hakikisheni mnafanya kikao kuona namna ya kulihamisha bomba hili kwani jambo hili si salama na pia baadhi ya mashirika ya ndege ya kimataifa yakibaini kama kuna uwepo wa bomba la gesi katika uwanja huu wanaweza kusitisha huduma zao”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Ametoa rai kwa watendaji wa Taasisi mbalimbali za Serikali kutochukua maamuzi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali kabla ya kushirikisha uongozi wa wilaya au mkoa kwa pamoja ili kupata ushauri wa maeneo ambayo yanafaa kwa ujenzi wa miundombinu hiyo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoka kukagua kivuko cha MV. Kilambo kinachotoa huduma kati ya kijiji cha Kilambo, mkoani Mtwara na Namoto, Msumbiji.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akikagua moja ya maboya kwa ajili ya usalama kwa watumiaji wa kivuko cha MV. Kilambo, kinachotoa huduma kati ya kijiji cha Kilambo na Namoto – Msumbiji. wakati alipofanya ziara yake mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akishiriki katika zoezi la uchanganyaji wa zege katika ujenzi wa barabara ya Tangazo-Kilambo yenye urefu wa KM 9.3, Mkoani Mtwara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...