Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) limekabidhi mashine tano za kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ‘cryotherapy machines’ mkoa wa Mwanza. 

Msaada huo umetolewa Jumanne Machi 27,2018 katika ukumbi wa mikutano wa Gold Crest Hotel jijini Mwanza wakati wa kikao cha wadau wanaohusika katika mapambano ya VVU na Ukimwi mkoani Mwanza kwa ajili ya kupanga mipango na mikakati ya kupambana na VVU na Ukimwi. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa alisema mashine hizo ni kwa ajili ya vituo vya afya vya Katunguru na Kabila vilivyopo wilaya ya Sengerema, hospitali ya Ngudu iliyopo wilayani Kwimba na zahanati ya Kirumba na kituo cha afya cha Buzuruga vilivyopo wilayani Ilemela. 

Dk. Sekela alisema mashine hizo tano zenye thamani ya shilingi milioni 6.8 zitatumika kutolea tiba mgando kwa akina mama wanaokutwa na dalili za mwanzo za kansa ya uzazi. “Mbali na shirika letu kuendelea kuboresha huduma za kinga na matunzo pia tunatoa huduma ya uchunguzi wa dalili saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama”,alieleza. 

Alisema huduma hiyo hutolewa katika vituo vya kutolea huduma ya afya 20 katika mkoa wa Mwanza. Dk. Sekela alisema shirika hilo mpaka sasa limetoa msaada wa ‘cryotherapy machines’ 17 katika mikoa sita ambayo ni Mwanza,Shinyanga,Tanga,Geita,Simiyu na Mara zote zikiwa na thamani ya jumla ya shilingi milioni 115.6. 

Dk. Sekela pia alikabidhi kompyuta 18 zitakazotumika kuhifadhi takwimu za wateja wa CTC katika vituo vya afya husika na kusaidia upatikanaji wa taarifa kwa haraka na kwa usahihi Zaidi mkoani Mwanza. “Tangu tuanze mradi wa Boresha, tutakuwa tumetoa jumla ya kompyuta 82 kwa mkoa wa Mwanza ambazo zinatumika kutunza taarifa za watu wenye VVU na Ukimwi”,alisema. 
Kulia ni Dk. Mwakyusa akiwa ameshikilia moja ya mashine inayotumika kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ‘cryotherapy machines’. 
Dk. Sekela akizungumza ukumbini. 
Katikati ni Dk. Sekela Mwakyusa akikabidhi mashine kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza,John Mongella (wa pili kushoto) na viongozi wa wilaya ya Sengerema. 
Zoezi la makabidhiano likiendelea. Wa kwanza kushoto ni Mwakilishi wa CDC nchini, Dk. Eva Matiko. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...