Jumatatu Aprili 9, 2018; Tanzania imepata wawakilishi wawili watakaoshiriki katika msimu
wa saba wa tuzo maarufu barani Afrika kwa wanafunzi wapenzi wa masomo ya Sayansi na
Teknolojia ijulikanayo kama - DStv Eutelsat Star Awards. Wanafunzi hao Michael Ditrick wa
shule ya Sekonday Ilboru – Arusha na Taher Rasheed wa Al-Madrasat Ussaifiyatul
Burhaniyah ya jijini Dar es Salaam
Michael ameshika nafasi ya kwanza katika uandishi wa insha maalum na Taher kwa mchoro
maalum kuhusiana na sayansi ya Setelait ambapo wanafunzi zaidi ya 150 kutoka shule
mbalimbali nchini walishiriki katika mashindano hayo ya mwaka huu. Washindi hao
walipatikana kutakana na utahini uliofanywa na jopo la majaji sita.
Kazi za washindi hao zimewasilishwa MultiChoice Africa ambapo zitapambanishwa na kazi
kama hizo kutoka kwa washindi wa nchi nyingine kote barani Afrika na hatimaye kupatikana
mshindi wa jumla katika kila kipengele yaani wale walioandika insha na wale walioandaa
mchoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Maharage Chande, amesema tuzo za
mwaka huu zimekuwa na ushindani mkubwa ambapo shule kutoka mikoa mbalimbali
ikiwemo Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Dodoma, Pwani zimeshiriki.
“Kuongezeka wa idadi ya wanafunzi wanaoshiriki katika tuzo hizi ni ishara njema na
tunaamini kwa viwango walivyoonyesha, bila shaka mwaka huu tutapata ushindi mkubwa
kuliko hata ule wa mwaka jana” alisema Maharage.
Amesema tuzo hizi zinalenga kuwajengea vijana wetu ari ya kushiriki katika masomo ya
sayansi na pia kuhamasisha ubunifu na ugunduzi katika tasnia ya sayansi. Amewataka
walimu kuwahimiza wanafunzi wao kushiriki katika tuzo kama hizi za kimataifa kwani ni
kipimo kizuri kwa wanafunzi wetu na pia inajenga kujiamini kwa wanafunzi wetu.
Tuzo hizi ambazo zinahusisha uandishi wa insha maalum au kuandaa bango vyenye ujumbe
kuhusiana na elimu ya anga hususan Setelait ni za wazi kwa wanafunzi wote wa shule za
sekondari wenye umri kati ya miaka 14 – 19.
Mwaka huu, washindani walitakiwa kuandika insha au kubuni bango kuhusu manufaa
yaliyoletwa na uvumbuzi wa setelaiti katika maisha ya kila siku hapa ulimwenguni na ni jinsi
gani setelait imekuwa kama kiungo muhimu kwa shughuli zote zinazofanyika kote duniani.
Kama kawaida tuzo hizi zina zawadi kabambe ambapo mshindi wa Insha atapata fursa ya
kuzuru kituo cha Eutelsat nchini Ufaransa na pia kwenda Guiana kushuhudia mubashara
urushwaji wa setelait angani.
Mshindi wa bango atajishindia safari ya kwenda nchini Afrika Kusini na kutembelea kituo cha
anga cha nchi hiyo na pia makao makuu ya MultiChoice Africa akiwa kama mgeni maalum.
Shule zitakazotoa washindi hao zitapata zawadi ya kufungia huduma ya DStv bure.
Wanafunzi wengine waliofanya vizuri katika mchakato huo ni pamoja na Pio Mwita wa
UWATA Sekondari ya Mbeya ambaye ameshika nafasi ya pili kwenye insha na Peter Kiama
wa Feza Boys ya Dar es Salaam aliyeshika nafasi ya pili kwa upande wa bango.
Mwaka jana Tanzania iliibuka mshindi wa pili kwenye insha baada ya Davids Bwana wa
FEZA Boys kunyakua nafasi hiyo nyuma ya mwanafunzi Leoul Mesfin kutoka Ethiopia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...