*Ni kutokana na juhudi za Serikali za kuhamasisha kilimo cha pamba 

ZAO la pamba ni miongoni mwa mazao makubwa ya biashara yaliyokuwa yakiliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni na kuchangia kukuza uchumi wa wananchi miaka ya 1970.

Kwenye miaka ya 1970 kulisheheni vyama vingi vya ushirika wa zao la Pamba na viwanda vya kuchambua nyuzi na kukamua mafuta, ambavyo vilibadili  hali halisi ya kipato cha wananchi wa eneo linalolimwa zao hilo na kulifanya kujulikana kama dhahabu nyeupe.

Kilimo hicho kilianza kudorora miaka ya hivi karibuni kutokana na kulegalega kwa vyama vya ushirika na matokeo yake pamba iliuzwa ikiwa chafu bila kuzingatia ubora  na madaraja yaliyopo.

Kutokana na sababu hizo Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, iliamua kufufua zao hilo ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi ya viwanda vya nguo na mafuta yatokanayo na mbegu za pamba zinapatikana pamoja na kuinua uchumi wa wakulima nchini.
 Katika kufanikisha suala hilo Serikali ilianza kwa kuwaagiza viongozi wa mikoa yote inayolima pamba kuhakikisha wanawahamasisha wakulima kufufua mashamba yao na ilihakikisha inafuatilia jambo hilo kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba, ugawaji wa pembejeo hadi utafutaji wa masoko.

Baada ya kutoa agizo hilo ambalo lilifanyiwa kazi na tayari mafanikio yameanza kuonekana katika msimu wa mwaka huu, kwa wakulima  kuanza kuvuna na kuuza kwa mafanikio.

Akizungumzia kuhusu hali ya zao hilo mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella, anasema msimu wa mwaka huu umekuwa na mafanikio makubwa kutokana na hamasa iliyotolewa na viongozi wakuu wa Serikali.
 Bw. Mongella anasema kutokana na hamasa hiyo, mwaka huu wanatarajia kupata mavuno makubwa kutoka katika kilimo  hicho kwa sababu wakulima wengi wamelima na baadhi yao tayari wameshaanza kuvuna.

Anasema Rais Dk. Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, walitoa maelekezo mahususi na walifanya ufuatiliaji wa karibu wa kilimo cha mazao makuu matano ya biashara nchini, likiwamo na zao la pamba.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya zao hilo jijini Mwanza hivi karibuni, Bw. Mongella amesema zao la pamba litasaidia kufufua viwanda vya mafuta ya kula, nguo pamoja na kuongeza ajira.

Amesema baada ya Rais Dkt. Magufuli kuhamasisha kilimo cha zao hilo, ambacho kilianza kusuasua nchini, viongozi waliitikia na kuwahimiza wakulima wachangamkie fursa hiyo, ambao walikubali.
 “Tunashukuru kwa hamasa na miongozo iliyotolewa na viongozi wetu kwa sababu iliongeza ari kwa wakulima kulima zao la pamba kwa wingi na mwamko kwa wananchi kulima mazao mengine, likiwamo la mpunga,” anasema.

Hata hivyo, kiongozi huyo ameishukuru Serikali kwa kuagiza pamba itakayovunwa iuzwe kupitia minada itakayosimamiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) katika kila eneo, jambo ambalo limesaidia  kufufuka kwa vyama hivyo.
“Tunashukuru kwa maelekezo na miongozo iliyokuwa inatolewa na viongozi wetu wakuu. Sasa AMCOS zetu zimefufuka na huu ni mwanzo tu mapinduzi makubwa katika biashara ya zao la pamba na yajayo yanafurahisha zaidi,” anasisitiza Bw. Mongella.

Bw. Mongella anatarajia kuwahamasisha wakulima wote wa mkoa huo pamoja na wafugaji na wavuvi wajiunge katika AMCOS zilizoko katika maeneo yao, ili kuweza kuirahisishia Serikali kufanyanao kazi.

Mkuu huyo wa mkoa pia anatumia fursa hiyo kuwapongeza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maofisa Kilimo kuanzia ngazi ya wilaya hadi kijiji na wakulima kwa kuhakikisha kilimo cha zao la pamba kinapata mafanikio.

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...