*Ni la wajawazito wanaosubiri kujifungua, limegharimu sh. milioni 129 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amenusa harufu ya ufisadi katika mradi wa ukarabati wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma (HOMSO) na amesema kwamba hajaridhishwa na kiasi ya sh. milioni 129 zilizotumika.

Hivyo, amemuagiza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile afuatilie suala hilo ili kumbaini mtu ambaye amehusika katika kupitisha zabuni ya ukarabati wa jengo hilo na kisha kumpelekea taarifa.

Waziri Mkuu amenusa harufu ya ufisadi katika mradi huo leo (Jumamosi, Januari 5, 2019) wakati alipotembelea hospitali hiyo na kukagua ukarabati wa jengo la akinamama wajawazito wanaosubiri kujifungua (mama ngojea) ambalo umegharimu sh. milioni 129.

“Sijaridhishwa na gharama za ukarabati wa jengo hilo kutokana na kiasi kikubwa cha fedha kilichotumika kwani Serikali inajenga vituo vya afya vyenye jengo la maabara, jengo la kujifungulia, wodi ya mama na mtoto, chumba cha upasuaji, nyumba ya watumishi kwa gharama za sh. milioni 400 hadi 500 sasa inawezekajane jengo moja linalokarabatiwa ligharimu kiasi hicho.”

Waziri Mkuu amesema kila mtumishi wa umma lazima azingatie maadili ya kiutumishi na kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na Serikali. Amesema Serikali imeagiza miradi ijengwe kwa kutumia force accountna kuhakikisha miradi inalingana na thamani ya fedha.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia kikamilifu utoaji wa huduma ya watoto waliochini ya miaka mitano zinazotolewa katika hospitali kwani baadhi ya wahudumu wa afya wamekuwa wakiwatoza gharama za dawa wakati wanatakiwa watibiwe bure.

Waziri Mkuu amesema hayo baada ya Kanisia Fusi ambaye amelazwa na mtoto wake katika hospitali hiyo kumueleza kwamba ameandikiwa dawa na kuambia akanunue wakati mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu anatakiwa atibiwe bure.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...