

Washiriki wa Mkutano wa NHIF na Wanahabari wa Kigoma wakifuatilia ufafanuzi wa hoja zinazohusu huduma za Mfuko.
Meneja Uhusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Anjela Mziray akizungumza katika mkutano wa Mfuko na Wanachama wa Chama cha Wanahabari wa Mkoa wa Kigoma.

Kaimu Meneja wa NHIF Kigoma, Bw. Emmanuel Kileo akiwasilisha mada kwa wanahabari wa Mkoa wa Kigoma.

Washiriki wa Mkutano wa NHIF na Wanahabari wa Kigoma wakifuatilia ufafanuzi wa hoja zinazohusu huduma za Mfuko.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Mkoa wa Kigoma, Bw. Deogratius Nsokolo akifafanua jambo juu ya mchango wa wanahabari katika utekelezaji wa shughuli za Mfuko.

Picha ya pamoja kati ya Maofisa wa NHIF na Wanahabari wa Mkoa wa Kigoma
……………………………………………………………………………….
Na Grace Michael, Kigoma
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) umeimarisha utekelezaji wa majukumu na kurahisisha huduma kwa
uwekezaji kwenye mifumo ya TEHAMA inayomwezesha mwanachama kupata huduma
kwa haraka zaidi pamoja na Watoa huduma kuwasilisha madai yao kwa
haraka.
Maboresho haya yamefanyika na
yanaendelea kufanyika kwa lengo la kuwarahisishia wanachama upatikanaji
wa huduma na kuondokana na changamoto ambazo awali zilikuwepo za
ucheleweshaji wa huduma mbalimbali ikiwemo utoaji wa vitambulisho na
upatikanaji wa taarifa za wanachama.
Akizungumza katika mkutano baina
ya NHIF na Wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Kigoma,
Meneja Uhusiano wa Mfuko, Bi. Anjela Mziray alisema kuwa uimarishaji wa
mifumo ya huduma unaofanywa na Mfuko umewezesha kutatua changamoto za
upotevu wa muda kwa wanachama wanapokuwa vituoni, kurahisisha utambuzi
wa mwanachama kabla ya huduma, lakini pia kurahisisha uwasilishaji na
ulipaji wa madai ya Watoa Huduma.
“Lengo la Mfuko ni mwanachama
wetu apate huduma kwa haraka na aweze kuwasiliana nasi kwa haraka
anapohitaji, uimarishaji huu wa Mifumo ambao umefanyika na unaoendelea
kufanyika, kwanza kabisa unawezesha upatikanaji wa taarifa za wanachama
kwa haraka wanapokuwa katika vituo vya kupata huduma na inapotokea
changamoto yoyote inatatuliwa kwa haraka zaidi tofauti na awali,”
alisema Bi. Mziray.
Alieleza kuwa Mfuko sasa
unaendelea na jitihada za kuwaunganisha watoa huduma wengi zaidi na
mifumo hiyo ili waweze kuwasilisha madai yao kila siku mara huduma
inapotolewa kwa mwanacha bila kusubiri mwisho wa mwezi. Hii inasaidia
kushughulikia dai la mtoa huduma kila linapowasilishwa na hivyo
kupunguza muda unaotumika kuchakata madai na hivyo kuongeza ufanisi.
“Kwa sasa tayari kuna baadhi ya
Watoa huduma ambao wameanza kutumia mfumo wa uwasilishaji wa madai kwa
Mfuko kila siku na hatua hii mbali na kurahisha malipo lakini pia
inaziba mianya ya udanganyifu na kuwezesha ulipaji wa madai halali
yaliyotumiwa na wanachama,” alisema Bi. Mziray.
Akizungumzia suala la kuongeza
wigo wa wanufaika wa huduma za NHIF, alisema kuwa Mfuko kwa sasa uko
katika hatua za mwisho za kuanzisha utaratibu ambao utawezesha watu
wengi kujiunga na kunufaika kwa namna mbalimbali kulingana na mahitaji
yao.
“Mipango yetu ni kuhudumia
asilimia 50 ya wananchi ifikapo mwaka 2020 na badae kuwafikia wananchi
wote hivyo maboresho na uimarishaji wa huduma tunaoufanya ni kujipanga
na utoaji wa huduma kwa wananchi wote ili kila mtanzania aweze kupata
huduma za matibabu kwa utaratibu rahisi wa bima ya afya,” alisema Bi.
Mziray.
Naye Kaimu Meneja wa NHIF Mkoa wa
Kigoma, Bw. Emmanuel Kileo alisema kuwa uwepo wa Ofisi ya NHIF mkoani
hapo imesaidia kwa kiasi kikubwa kusogeza huduma kwa wananchi ambapo kwa
sasa maofisa wa Mfuko wanawafikia wananchi mpaka ngazi ya kijiji na
kuwapatia elimu ya umuhimu wa kujiunga na huduma.
Wakichangia hoja juu ya huduma za
Mfuko, wanahabari wa Mkoa wa Kigoma, wameupongeza Mfuko kwa jitihada
kubwa ambazo zimefanyika hususan katika kuyafikia makundi mbalimbali na
kuboresha huduma za matibabu kwa wanachama wake.
Akitoa shukrani kuhitimisha
mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Kigoma Bw. Deogratius
Nsokolo alisema watauendeleza uhusiano uliopo baina yao na Mfuko huu
hususan katika kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na bima ya
afya kabla ya kuugua.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...