*Habari nyingi ni za matukio, za kuikosoa Serikali haziandiki
Na Karama Kenyunko,Globu ya jamii
RIPOTI
ya matokeo ya Utafiti kuhusu Ubora wa Maudhui ya vyombo vya habari
Tanzania kwa mwaka 2018 unaonesha ni nadra kwa vyombo vya habari
kuandika au kutangaza habari zenye kuikosoa Serikali huku pia ikionesha
kuwa ubora wa kuripoti habari uko chini na nyingi ni za matukio.
Pia
ripoti hiyo inonesha kumekuwepo na dhana kwamba vyombo vya habari
vinaripoti zaidi habari zinazotoka katika miji mikubwa ikiwemo ya Dar es
Salaam,Dodoma, Mwanza, Mbeya,Arusha,Mjini Magharibi na Kusini Pemba.
Kwa
mujibu wa watafiti wa utafiti huo ambao ni Christoph Spurk kutoka
Switzerland na Abdallah Katunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
kupitia Spurk Media Consulting Ltd wamesema vyombo vya habari vinawajibu
mkubwa wa kuhamasisha maendeleo kwa kutoa habari zenye weledi, maslahi
kwa umma na zenye kuwasamamia wenye mamlaka kuhakikisha wanatenda
kulingana na taratibu zilizowekwa.
Hata hivyo wamesema wajibu huo
muhimu unaweza kutimizwa na kuendelezwa pale tu vyombo vya habari
vinapoweza kuripoti kwa kufuata vigezo vya kitaaluma na kwamba utafiti
huo wa ubora wa vyombo vya habari Tanzania mwaka 2018 umechambua ubora
wa vyombo vya habari kwa kutazama namna vinavyoripoti habari zao kwa
kutumia vigezo maalumu ambavyo vimekubaliwa na wadau wa vyombo hivyo.
Akifafanua
zaidi, Mtafiti Abdallah Katunzi amesema jumla ya sampuli 1886 ambazo
zinajumuisha habari, makala na maoni kwa upande wa magazeti, habari na
vipindi vya redio na televisheni pamoja na posti za blogu na mtandaoni
kutoka vyombo vya habari 25 Tanzania Bara na Zanzibar na kwamba vyombo
hivyo vinajumuisha magezeti saba , redio za kitaifa tano, redio za
mikoani saba, televisheni za kitaifa tatu, televisheni ya mtandaoni
moja, blogu moja na mitandao moja.
"Kwa ujumla matokeo yanaonesha
ubora wa kuripoti kwa vyombo vya habari nchini uko chini kwenye vigezo
vingi vilivyotazamwa kwa upande wa vigezo vya kitaaluma zaidi ya 1/3
ambapo asilimia 36 ya sampuli yote iliyochambuliwa imetumia chanzo
kimoja cha habari na kwamba habari habari nyingi za waandishi ni zao la
habari za matukio kwa asilimia 60 ikiwa ni ongezeko la asilimia nane
ukilinganisha na matokeo ya utafiti wa mwaka 2017, ingawa kuna tofauti
kubwa kati ya aina ya habari na vyombo vya habari,"amesema Katunzi.
Ametoa
mfano kuwa za magazeti ni zao la habari za matukio kwa asilimia 72
wakati makala zinazozalishwa kwa kutegemea jitihada ya vyombo husika ni
kwa asilimia 85 na kwamba upande wa televisheni asilimia 78 ya habari ni
zao la habari za matukio wakati asilimia 90 ya vipindi vinazalishwa nje
ya mfumo wa kufuata matukio.
Pia amesema kuna tofauti kubwa
miongoni mwa vyombo vya habari, gazeti la Jamhuri lililofanya vizuri kwa
mwaka 2018 habari zake zinatokana na jitihada za wahandishi kutafuta
habari hizo kwa asilimia 63 wakati gazeti la The Gurdian ni asilimia 19
pekee.
Katunzi amesema kuwa ukitazama vigezo vya ukamilifu wa
habari matokeo pia siyo mazuri kwa wastani ni asilimia 23 tu ya habari
,vipindi na makala zilizochambuliwa ndio zilikuwa na maelezo ya kwanini
habari hizo zimeandikwa(root causes).Wakati asilimia tisa pekee ya
sampuli yote ndio imeweza kutoa usuli(back ground) wa habari
zilizoandikwa.
Kwa upande wa habari kueleweka kwa walengwa ,
amesema hali inaridhisha kwani asilimia 56 ya kazi zote zilizochambuliwa
zina muundo mzuri wa waandishi huku zikiunganisha sehemu mbalimbali za
habari kwa mtiririko mzuri.Hata hivyo bado kuna changamoto kwa vyombo
vya habari kuelezea takwimu kwa namna ambayo inamsaidia msomaji au
msikilizaji kuzielewa takwimu hizo ni asilimia 25 pekee ya kazi zote
ndio imeweza kuelezea takwimu kwa kumrahisishia mlengwa kuzielewa.
Kuhusu
maadili, amesema asilimia 42 ya sampuli yote imeshindwa kuwapa nafasi
watuhumiwa kujieleza ikilinganishwa na asilimia 60 za mwaka 2017 ,
magazeti yamezingatia kigezo hicho kwa asilimia 50 huku redio na
televisheni kwa asilimia 33 mutawalia. "Kuna tofauti kubwa kati ya redio
au televisheni na magazeti na chombo kimoja kimoja cha habari.Kwa
ujumla magazeti yamefanya vema kwenye vigezo vingi ukilinganisha na
televisheni na redio, magazeti kwenye vigezo vyote kwa asilimia 33.2.
Pia
amesema utafiti unaonesha kuwa ni vyombo vya habari vichache ndio
vinaandika habari za kukosoa utendaji wa Serikali na katika eneo hilo ni
Jamii Forums ndio inamaudhui ya kukosoa utendaji wa serikali.
Kupita
utafiti huo inapendekezwa ili kuimarisha ubora wa vyombo vya habari
inapendekezwa vyombo hivyo vitumie matokeo ya tafiti hiyo na hasa
vikijikita kwenye maeneo ambayo havijafanya vizuri au viko chini ya
wastani.Hata hivyo vyombo vya habari vinapaswa kujiimarisha kwenye
maeneo kama ujumuishaji wa usuli kwenye habari.
"Sababu za
kuandikwa kwa habari husika na kuongeza idadi ya habari ambazo
zitachochea utendaji kazi wa Serikali ili kuvisaidia vyombo vya habari
kujitathimini vyenyewe, utafiti wa mwaka 2018 umeboresha pima kadi ya
ubora wa habari ambayo kwa sasa redio za mikoani inaonesha matokeo kwa
kila kigezo kwa kulinganisha na wastani na alama ya juu.Pia utafiti huu
umetayarisha pima kadi nyingine ambayo inaonesha nafasi ya kila
chombo,"amesema Katunzi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...