Na Mwandishi Maalum – JKCI
Jumla ya watu 62 wamefanywa vipimo vya kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echo Cardiogram) na umeme wa moyo (ECG) wakati wa
punguzo la gharama za matibabu kwa wagonjwa wa kulipia lililotolewa na
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Punguzo hilo lilitolewa hivi karibuni na Taasisi hiyo ikiwa ni sehemu
ya kusherehekea ushindi wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa
kuifunga timu ya Uganda mabao 3-0 na kuweza kushiriki katika
mashindano ya Taifa Bingwa Barani Afrika AFCON. 2019.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam Mkurugenzi
wa Kurugenzi ya Tiba Shirikishi ambaye pia ni daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo Dkt. Delila Kimambo alisema kati ya wagonjwa 62
waliopima afya zao nane walikuwa ni watoto.
Dkt. Delila alisema katika kusherehekea ushindi wa timu ya Taifa
Taasisi hiyo imeona ni vyema kufungua milango na kuwahamasisha
wananchi kujitokeza kupima afya ya moyo.
“Kati ya watu 62 tuliowapima 19 tuliwakuta na matatizo ya moyo ambapo
wa nne wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo,
mmoja kati yao ameshafanyiwa na kukutwa na tatizo la kuziba kwa
mishipa miwili ya damu ameshazibuliwa mshipa mmoja na anaendelea
vizuri”,.
“Wengine wanne walikutwa na tatizo la valvu ambapo wawili wanatakiwa
kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha valve. Wengine tumewakuta na
shinikizo la juu la damu”,.
“Zoezi hili limefanyika vizuri, tunafahamu kuwa kuna wananchi ambao
huwa wanahitaji vipimo vya moyo kwa dharula na hawawezi kufika kwetu
kutokana na shida mbalimbali za maisha, hivyo tulitoa punguzo hili la
bei ili kuwafungulia milango ya kupata matibabu ya vipimo vinavyoweza
kugundua kama mtu ana magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Delila.
Dkt. Delila alimalizia kwa kuwaomba watanzania kuwa na utamaduni wa
kupenda kupima afya zao mara kwa mara ,kupata matibabu na majibu ya
magonjwa yanayowasumbua kutoka kwa wataalamu wa magonjwa husika.
Kwa upande wake Frank Karia ambaye ni makazi wa Mwanza alisema alipewa
Rufaa kutoka hospitali ya rufaa ya Bugando na kufika JKCI siku ya
Jumatatu ambapo kulikuwa na punguzo la bei na kubahatika kufanyiwa
vipimo vya ECHO na ECG baada ya kufanyiwa vipimo aligundulika kuziba
kwa mishipa miwili inayopeleka damu kwenye moyo.
“Baada ya kukutwa na tatizo ndani ya wiki moja tayari nimeshazibuliwa
mshipa mmoja wa damu na hali yangu inaendelea vizuri kama unavyoniona,
baada ya wiki mbili nitarudi kliniki . Leo tarehe
29/03/2019nimeruhusiwa kwenda nyumbani, kwa kweli sikutegemea kama
ningepata huduma hii kwa kipindi cha wiki moja” alisema Karia.
Alisema huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo ni za kimataifa na
kuwaomba waendelee kutoa elimu kwa umma ili wananchi wafahamu zaidi
huduma zinazotolewa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...