Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki ya Exim Tanzania Bw Stanley Kafu (Kulia) akipokea tuzo maalum kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ikiwa ni utambuzi wa mchango wa benki hiyo katika kufanikisha suala la uhamasishaji na uchangiaji wa damu salama hapa nchini katika Maadhimisho ya Siku ya Wachangiaji Damu Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza mwishoni mwa wiki.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Exim Tanzania kutoka makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Hazina na Masoko ya Fedha wa benki hiyo, Bw Arafat Haji (katikati) wakichangia damu katika Maadhimisho hayo.
Pamoja na wafanyakazi pia baadhi ya wateja wa benki hiyo walijitokeza kwa wingi makao makuu ya benki hiyojijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujitolea damu.


  Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine Ulimwenguni katika kuadhimisha Siku ya Wachangiaji Damu Duniani, Benki ya Exim Tanzania imekabidhiwa tuzo maalum kutoka serikalini ikiwa ni utambuzi wa mchango wa benki hiyo katika kufanikisha suala zima la upatikanaji wa damu salama hapa nchini.

Benki hiyo imekabidhiwa tuzo hiyo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu katika Maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, viwanja vya Furahisha mwishoni mwa wiki iliyopita yakiwa na kauli mbiu ‘Damu Salama Kwa Wote’

Akiipongeza benki hiyo kwa ushiriki wake mkubwa kwenye jitihada za upatikanaji wa damu salama hapa nchini, Waziri Ummy ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo pia aliihimiza benki hiyo kuendelea kuwa balozi imara wa damu salama hapa nchini sambamba na kuhamasisha taasisi nyingine na watu binafsi kuungana na benki hiyo katika kufanikisha mpango huo muhimu.

“Serikali imetenga Sh. bilioni tano katika mwaka wa fedha 2019/20 zitakazotumika kujenga vituo vidogo vya uchangiaji damu salama katika mikoa 12 nchini.’’ Alisema Ummy ambae pia alizindua mashine mpya ‘full automation’ za kupima maambukizi katika damu na za kupima makundi ya damu ambazo zimesimikwa kwenye vituo vya kanda sita ikiwamo Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Mtwara na Mbeya.

“Tunataka kumfikia kila mtanzania mwenye mahitaji ya damu salama popote alipo tuhakikishe anapata damu salama bila kikwazo chochote. WHO inakadiria idadi ya watu 1000 zipatikane chupa 10 za damu, Watanzania tunakadiriwa tupo milioni 55 tunapaswa kupata asilimia moja ya idadi hiyo, hivyo chupa 550,000 zinahitajika kila mwaka kutosheleza mahitaji,” alisema.

Akizungumza kuhusiana na tuzo hiyo Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Bw Stanley Kafu alisema: "Benki ya Exim tumepokea tuzo na heshima hii kutoka serikalini kwa mikono miwili kwa kuwa ni sehemu ya matokeo chanya ya mkakati wa benki ya Exim ya uwajibikaji kwa jamii unaofahamika kama ‘Exim Cares’. Hivyo tuzo na heshima hii ni kama chachu ya sisi kuendelea kujitoa zaidi katika kufanikisha mpango wa damu salama hapa nchini,’’ alisema

Kwa mujibu wa Bw Kafu, mapema mwezi huu benki hiyo kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) walianza utekelezaji wa pamoja wa mpango wa uchangiaji wa damu uliohusisha matawi yote ya benki hiyo hapa nchini hususani katika mikoa minane ya Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Tanga, Mtwara na Zanzibar.

"Sisi ni mojawapo ya taasisi ambazo zinaendesha huduma zake katika sehemu kubwa ya nchi hii na huduma yetu inagusa idadi kubwa ya watu. Tunaguswa na jamii tunayoihudumia na tunaamini jamii yenye afya ni muhimu katika kutimiza malengo yetu. Na hiyo ndio sababu tumeelekeza rasilimali zetu pamoja na maeneo ya ofisi zetu kama kambi za kukusanyia damu,’’ alisema Kafu

Benki ya Exim imeendelea kuonyesha uwajibikaji wake katika kusaidia sekta ya afya kupitia mipango mbalimbali na miradi ya kijamii. Katika miaka minane iliyopita benki imechangia zaidi ya chupa 1000 za damu katika Benki ya damu taifa.  



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...