*Yajibu za kero mbalimbali za Watanzania hasa wayonge

*Yaondoa utitiri wa kodi ...Waziri Mpango atoa muelekeo

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imesoma bajeti ya fedha kwa mwaka 2019/2020 kwa kutenga Sh. trilioni trilioni 33.

Dkt. Mpango wakati anasoma bajeti hiyo leo Bungeni Mjini Dodoma amefafanua kwa kina namna ambavyo Serikali imejipanga kuleta maendeleo ya Watanzania kupitia bajeti hiyo.

Akifafanua zaidi kuhusu bajeti hiyo yenye kurasa 71, Waziri Mpango amesema kuwa bajeti hiyo ni nyenzo ya kufikia matarajio ya wananchi wote.

"Hivyo, katika kuandaa bajeti hii, Serikali iliwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo, Kamati ya Bunge ya Bajeti, wafanyabiashara, taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi wa kawaida.

"Na wataalam wa kodi hususan wale walioshiriki vikao vya kazi vya kikosi kazi cha maboresho ya kodi kujadili na kushauri kuhusu mapendekezo ya maboresho ya kodi na tozo mbalimbali.

"Baadhi ya wadau walituletea maoni na ushauri kwa maandishi au barua pepe. Nakiri kuwa walitupatia mrejesho ambao umesaidia kuboresha será na vipaumbele  vya nchi yetu kwa mwaka 2019/20 na siku zijazo,"amesema.

Ameongeza kuwa kwa niaba ya Serikali wanashukuru kwa michango hiyo mizuri ambayo tumejitahidi kuizingatia na ni matarajio ya Serikali wadau hao wataendelea kufanya hivyo katika mchakato wa bajeti zitakazofuata.

Amesema kuwa bajeti ya 2019/20 inahusu kuendeleza juhudi za kujenga msingi wa uchumi wa viwanda ili kupanua fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi endelevu wa jamii  na hatimaye kuondokana na umaskini, ujinga na maradhi.

Amefafanua bajeti hiyo  imelenga kuimarisha na kujenga miundombinu ya kisasa ili kuongeza uwezo wa Taifa katika uzalishaji viwandani hasa vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini na kutoa huduma bora (afya, elimu na maji) kwa wananchi.

Aidha, miundombinu hiyo itasaidia kuongeza biashara nchini, kikanda na kimataifa kwa kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara na uwekezaji kwa kushughulikia changamoto zilizobainishwa katika mpango wa kuboresha mazingira ya biashara (Blueprint).

Pia kuimarisha kilimo (uzalishaji wenye tija na masoko ya mazao, ufugaji, uvuvi, na misitu) kwa kuzingatia umuhimu mkubwa wa sekta hii katika uchumi wa Taifa (chakula, ajira, kipato cha mwananchi, mchango katika fedha za kigeni na muunganiko wa sekta hii na maendeleo ya viwanda).

Ameongeza kuwa inalenga kudumisha amani na usalama katika Taifa; na kujenga misingi ya Taifa kujitegemea kiuchumi

Waziri Dkt. Mpango aliyesoma hotuba hiyo kwa zaidi ya saa mbili huku kukiwa na shangwe kutoka kwa wabunge wa CCM, amesema safari ya kuijenga Tanzania mpya imeiva lakini haitakuwa rahisi.

"Hasa tukizingatia mabadiliko yanayoendelea katika uchumi wa dunia, ushindani mkali wa kibiashara, mabadiliko ya haraka ya teknolojia na demografĂ­a na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

"Hata hivyo, bahati nzuri ni kuwa, katika historia ya nchi yetu, Watanzania ni watu jasiri katika mapambano dhidi ya changamoto zinazojitokeza na kila wakati zilipojitokeza tulizishinda  kwa kutumia ubunifu na nguvu ya umoja wa Watanzania.

"Hivi sasa tuko imara zaidi chini ya uongozi shupavu wa Dkt. John Joseph Magufuli. Uchumi wetu unaendelea kukua kwa kasi kubwa, ambapo mwaka 2018 ulikua kwa asilimia 7.0  na kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kinazidi kupungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18.

"Naamini pasipo shaka yoyote kwa umoja wetu, uongozi makini, kufanya kazi kwa bidii na kwa kutumia rasilimali za nchi yetu vizuri, tutaijenga Tanzania mpya, ambayo itakuwa kitovu kikuu cha uchumi (Economic hub) katika ukanda wa Afrika Mashariki katika muda usiozidi miongo miwili ijayo,"amesema Dk.Mpango.

Ametumia nafasi hiyo kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo kwa misaada na mikopo nafuu wanayoendelea kuitoa katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo nchini.

Amesema katika bajeti ya mwaka 2019/20, washirika wa Maendeleo kwa pamoja wanatarajia kuchangia jumla ya Sh.trilioni 2.78.

  Waziri Mpango amesema kwa kutambua uhusiano mzuri uliopo kati ya Serikali na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ni matarajio yao kuwa misaada ya kiufundi na fedha zilizoahidiwa na marafiki hawa zitatolewa kwa wakati na kwa kiasi kilichoahidiwa.

"Nasi kwa upande wa Serikali tunaahidi kutumia misaada hiyo kama ilivyokusudiwa.  Napenda nitumie nafasi hii kuwahimiza Mabalozi wanaoziwakilisha nchi  zao na taasisi za kimataifa hapa nchini Tanzania waongeze nguvu kukuza biashara kati ya nchi zao na nchi yetu na kuhamasisha wenye mitaji toka nchi zao kuja kuwekeza hapa Tanzania.

"Tanzania ni salama kwa uwekezaji wenye faida kwao na kwetu. Aidha, wafanye jitihada zaidi kuhamasisha watalii kuja kujionea vivutio vya utalii, ambavyo ni fahari ya Tanzania,"amesema.

Pia amesema Serikali ya Awamu ya Tano inatambua na kuthamini michango yao katika maendeleo ya Taifa letu ili mradi isiambatane na masharti yanayohatarisha uhuru wa Tanzania (national sovereignity),

Ameongeza au kwenda kinyume na mila na desturi zetu na kwamba hata pale ambapo Serikali au mihimili mingine imefanya maamuzi ambayo hawakubaliani nayo, ni vema na haki washirika wetu wa maendeleo wakatoa muda wa kuyatafakari na kujadiliana nao kwa staha badala ya kuishinikiza Serikali ibadili uamuzi wake ndipo watoe fedha, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo.

Waziri Mpango amewasisitiza Watanzania kuendelea kushikamana katika kuijenga Tanzania mpya na kuwa wazalendo na wakae macho daima kulinda na kutetea maslahi ya Taifa letu.

"Tuongeze bidii kufanya kazi. Enzi za kutegemea wajomba hazipo tena na habari njema ni kuwa: “Tukiamua Tunaweza” na Serikali ya CCM inayoongozwa na Dkt. John Magufuli imethibitisha ukweli huo.

"Naomba kwa niaba ya Serikali kupongeza mchango mkubwa wa wafanyabiashara na wananchi wote ambao wamelipa kodi kwa mujibu wa sheria. Pia natambua mchango adhimu wa mashirika na taasisi ambazo Serikali ina hisa yaliyotoa gawio au asilimia 15 ya mapato ghafi kuingia katika Mfuko Mkuu wa Hazina,"amesema.

Amefafanua katika mwaka ujao wa fedha, Serikali inayataka mashirika yote ya umma na taasisi ambazo Serikali ina hisa kuhakikisha kuwa wanatoa gawio au mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi na Msajili wa Hazina asimamie kikamilifu utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali.

Wakati huo huo amesema Oktoba mwaka huu wa 2019 nchi yetu itafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo Serikali kwa upande wake imejipanga kikamilifu katika maandalizi ikijumuisha mahitaji ya kibajeti kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo.

"Ninawasihi wananchi wote wenye sifa wajitokeze kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura. Aidha, katika kuchagua viongozi wa ngazi hiyo, tafuteni Watanzania wenye sifa,"amesema.

Amezitaja baadhi ya sifa hizo ni awe mchapakazi mwenye kujitoa sadaka kuwatumikia watu, hasa wananchi wa kawaida, mwepesi kuona, kusikiliza na kuguswa na shida za wananchi wake na tena awe jasiri katika kupigania haki za wanyonge na awe na uwezo na ubunifu katika kutatua kero za wananchi hao.

Pia awe mwadilifu, anayechukia na kupiga vita rushwa na ufisadi kwa matende, anayetambua fursa zilizopo katika eneo lake, kubuni mikakati ya kuwaendeleza wananchi anaowaongoza na kuwatia watu wake hamasa ya kuthubutu kutumia fursa hizo;

Sifa nyingine awe mtetezi hodari wa kulinda mazingira na mpambanaji dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, mwenye kutoabudu nyadhifa na anayetambua kuwa nafasi na vyeo tulivyopewa ni vya muda tu. Ni vya kupita!

"Thamani halisi ya kiongozi ni kufanya kazi kwa bidii na kuacha kumbukumbu nzuri kwa ustawi wa eneo analoliongoza na Taifa kwa ujumla.

"Awe kama mchezaji mzuri wa kiungo katika timu ya ushindi, anayetambua kwamba mkono mmoja hauwezi kupiga makofi ya shangwe, awe mwenye kutambua kazi za kiongozi zina maana sana kwa kuwa zinamwezesha kubadilisha maisha ya maelfu ya Watanzania, hasa wanyonge, kuwa bora zaidi;

"Pia awe na uwezo wa kuwaeleza wananchi kinaganaga kuhusu Serikali yao inawapeleka wapi na wajibu wa kila mmoja ili waendelee kuiunga mkono; na awe anatoka ndani ya chama cha siasa kinachotetea maslahi na haki za wanyonge na chama hicho ni CCM,"amesema.

Dk.Mpango amekiri kuwa, sifa hizi alizozitaja  ameziazima kutoka kwa Dkt. John Magufuli, bila ridhaa yake na kutumia nafasi hiyo kuomba viongozi wote wa dini pamoja na waumini wote kila mmoja kwa imani yake, tuendelee kumwombea Rais.

 "Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia afya njema, hekima, busara na kumwongoza kwa kila jambo alifanyalo kuliletea Taifa letu maendeleo,"amesema Dk.Mpango.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango akiwasili katika viwanja vya  Bunge kwa ajili ya kusoma Bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2019/2020 Jijini Dodoma, Juni 13.2019. 
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, akisoma Bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2019/2020, Bungeni jijini Dodoma Juni 13, 2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...