Promosheni ya kusherehekea maadhimisho ya miaka 5 ya MPAWA iliyokuwa ikiendeshwa na Benki ya CBA na kampuni ya Vodacom imefika tamati leo huku kukishuhudiwa mshindi aliyeibuka na zawadi ya Tsh Milioni 15 na wengine 339 wakiondoka na mara 2 ya akiba yao, Simu kali na muda wa maongezi katika droo ya mwisho iliyofanyika leo asubuhi.

Droo hiyo kubwa na ya mwisho iliendeshwa kwenye makao makuu ya benki ya CBA yaliyopo Posta jijini Dar es salaam mbele ya Afisa kutoka Bodi ya Michezo ya bahati nasibu, Bw. Humudi Abdal Hussein, Wawakilishi kutoka Benki ya CBA Yessie Yassin na Maria Marbella, Mwakilishi kutoka Kampuni ya Vodacom Bi. Alice Lushiku, watangazaji maarufu Dokii na Mpoki ambao pia ni mabalozi wa huduma hiyo ya MPAWA pamoja na waandishi wa habari.

Promosheni hii iliyokuwa inawalenga watumiaji wote wa MPAWA nchi nzima ilianzishwa kwa ajili ya kuwajumuisha wateja wote kifedha, kuwawezesha wateja kutengeneza utamaduni wa kuweka akiba, kukopa na kurudisha mkopo mapema iliendeshwa kwa muda wa wiki 6 na ilianza na watumiaji zaidi ya 1000 kuibuka washindi wa zawadi mbalimbali ikiwemo mara 2 ya akiba yao kuanzia Shilingi 1000 – 200,000, simu janja na muda wa maongezi kila wiki. Washindi walichaguliwa kwa vigezo mbalimbali ikiwemo kuweka akiba, kurudisha mkopo mapema na chalenji ya kuweka akiba na mshindi mkubwa aliyetangazwa leo aliyeshinda zawadi ya Mil 15.

Andrisa Mathias miaka 27 kutoka Geita ndiye aliibuka mshindi mkubwa wa promosheni hii kubwa ya Miaka 5 ya MPAWA akiondoka na Sh Milioni 15 za kitanzania huku washindi wengine wakiondoka na mara 2 ya akiba yao ndani ya akaunti zao za MPAWA.

Akiongea na waandishi wa habari, Mwakilishi Mkuu wa MPAWA benki hiyo ya CBA, Bibi. Gloria Njiu alisema “MPAWA ni huduma inayolenga kuwaendelea na kuwawezesha watanzania wengi hususani wasiofikiwa na huduma za kibenki pamoja na wajasiriamali wadogo, na maadhimisho haya ya miaka 5 yanalenga kuwawezesha na kuwashukuru wapendwa wateja wetu wote.” Aliongezea kuwa Benki ya CBA inajivunia safari hii ya miaka hii 5 ya mafanikio ya huduma hii na kuwapongeza wateja wote walioshinda hususani Andrisa ambaye ni mshindi mkubwa wa promosheni hii.

Akiongea kwa njia ya simu, mshindi huyo wa Milioni 15 alionesha furaha za waziwazi na kutoa shukrani zake kwa benki ya CBA na kampuni ya Vodacom kwa kuanzisha huduma hii na promosheni hii ya kuwazawadia wateja wake. Aliongezea kwa kuzipongeza taasisi zote mbili kwa kuwawezesha wateja wake kupitia kampeni hii ya Miaka 5 ya MPAWA na kuahidi kuendelea kuwa mtumiaji mzuri wa huduma hii kutokana na faida zake.

Mwakilishi kutoka kampuni ya Vodacom, Bi.Alice Lushiku pia alitoa neno lake akisema “Tunawapongeza washindi wote na tunaendelea kuwahimiza waendelee kuhifadhi akiba zao, kurudisha mikopo yao mapema na kwa watu wote ambao sio wateja wa MPAWA tunawahimiza kujiunga na huduma hii inayowasadia kuwajumuisha katika ulimwengu wa kifedha hususani kwa watu ambao hawafikiwi na huduma za kibenki kwa urahisi.”

Bw Andrisa Mathias ambaye ni mshindi Milioni 15 atakabidhiwa zawadi yake Jumamosi hii kwenye hafla fupi itakayofanyika Lugalo , Dar es Salaam kuadhimisha miaka 5 ya huduma hii Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...