NA Moshy Kiyungi,Tabora.

Ukipima kwenye mizani historia ya muziki wa taarabu na tamaduni za unyago Visiwani Zanzibar, ni wazi kwamba mizani hiyo lazima itaegemea upande wa Fatuma Binti Baraka ‘Bi.Kidude’.

Uzoefu na uelewa aliokuwa nao katika fani hiyo, alikuwa hana mpinzani.

Nyimbo alizoimba miaka michache kabla ya kufariki dunia za ‘Muhogo wa Jang’ombe na ‘Halaiti’, zilimuongezea umaarufu zaidi.

Inaaminika kwamba Bi. Kidude ndiye aliyekuwa mwanamke, mwimbaji mkongwe kupita wote Afrika Mashariki na Kati.

Bi. Kidude alikuwa mwimbaji wa taarabu tangu miaka ya 1920, akiwa mfuasi wa Sitti Bin Saad.

Sitti alikuwa amebarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha uimbaji, alipokuwa akiimba sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali maili nyingi.

Alizaliwa mwaka 1880 katika kijiji cha Fumba huko Visiwani Zanzibar.

Sitti Binti Saad alikuwa mmojawapo wa waimbaji wa mwanzo kabisa wa taarabu Visiwani humo.

Bi. Kidude alizifuata nyayo za Sitti, akatambulika na kuheshimika kama Malikia wa taarabu na mambo ya unyago asiye na mpinzani.

Jina alilopewa na wazazi wake alipozaliwa ni Fatuma Binti Baraka.

Lakini baada ya kupata umaarufu katika uimbaji, jina la Bi. Kidude likashika nafasi.

Bi. Kidude alizaliwa katika kijiji cha Mfagimaringo katika familiya ya watoto saba.

Wakati wa uhai wake aliwahi kusema kuwa hafahamu mwaka aliozaliwa, kilichokuwa kinatamkwa na baadhi ya watu ni kwamba alikuwa na umri zaidi ya miaka 90 hadi alipofariki dunia.

Sio ajabu alikuwa ameshafikisha umri wa miaka 100!

Mtu yeyote iliyekuwa akimuuliza Bibi huyo kuhusu umri wake, alisema hawezi kuutaja, lakini alikuwa akitamka kuwa alizaliwa zama za sarafu ya rupia.

Rupia ilikuwa ni sarafu iliyotumiwa katika eneo la Afrika Mashariki mpaka wakati wa vita vya kwanza vya dunia.

Bi Kidude si kwamba alikuwa na mvuto kwa sauti yake nzuri ya kuimba taarabu, lakini pia namna ya muonekano wake katika jukwaa.

Wazazi wake walikuwa ni wafanyabiashara ya kuuza Nazi enzi hizo za Zanzibar iliyokuwa chini ya utawala wa Wakoloni wa Kiarabu.

Katika mahojiano mbalimbali aliyofanya na vyombo mbalimbali vya habari ulimwenguni, marehemu Bi.Kidude aliwahi kusema alianza kuimba akiwa na umri mdogo wa miaka kumi.

Alivutiwa sana na utunzi na uimbaji wa Sitti binti Saad, wakati huo yu ngali kigoli.

Fatuma Binti Baraka alikuwa akijificha nje ya nyumba ili kumsikiliza Sitti binti Saad akiwaimbia wageni ambao mara nyingi walikuwa wakipelekwa pale.
Akiwa na umri wa miaka 13, alionesha ujasiri mkubwa wakati alipotoroka katika visiwa vya Zanzibar, akakimbilia Tanzania Bara (Tanganyika enzi hizo), ili kuepuka kuozeshwa kwa nguvu kukwepa ndoa ya lazima.

Baadaye Bi. Kidudue akawa mtu anaejihusisha sana na muziki wa taarabu, alizunguka sehemu mbalimbali za nchi, akiwa mwimbaji katika makundi mbalimbali ya muziki huo likiwemo lile maarufu la Egyptian Musical Taarab.

Aliambatana na kundi hilo walipofanya ziara mbalimbali za muziki wa taarab katika maeneo ya Afrika Mashariki.

Fatuma Bint Baraka ‘alikwea Pipa’ akaenda nchini Misri, ambako aliimba huko kwa kipindi kifupi, akaamua kurejea Kisiwani Zanzibar.Aliporejea Zanzibar 1940, pamoja na kuwa mtu mwenye umaarufu mkubwa, aliendelea kuishi katika nyumba yake iliyotengenezwa kwa udongo.

Mbali na muziki alikuwa akijihusisha na vyama vya kijamii na Mwalimu wa ‘Unyago’ ambapo alikuwa na chuo chake akitoa elimu ya unyago kwa wasichana katika Visiwa hivyo.

Wakati wa uhai wake alikuwa akijivunia kwamba kati ya wanafunzi wake wote hakuna ambaye ameshawahi kupewa talaka na mumewe.

Pengine hii ndio sababu mwaka 2004 ulipozuka uzushi kwamba Bi.Kidude amefariki dunia wakati alipokuwa katika ziara ndefu ya kimuzik, kila mtu Kisiwani Zanzibar, alishikwa na butwaa na majonzi! .

Wakati wazushi ‘wanapakaza’ yeye alikuwa Ulaya na nchi za Mashariki ya mbali. Ikabainika kwamba habari za kifo chake zilikuwa ni uzushi mtupu.


Aidha Bi. Kidude alikuwa mjasiliamali akiuza Wanjana Hina ambazo alikuwa akizitengeneza mwenyewe pamoja na utaalamu wa dawa za mitishamba.

Mwaka 2005 huko Gateshead, Newcastle nchini Uingereza, Bi.Kidude alipokea Tuzo yenye heshima kutoka World Music Expo (WOMEX), kwa mchango wake katika muziki na Utamaduni wa Zanzibar.

Katika kinyang’anyiro hicho aliwashinda wanamuziki mahiri kama Peter Gabriel, Miriam Makeba na wengineo.

Bi. Kidude aliwahi kusema kwamba hawezi kuacha kuimba mpaka siku atakapoiaga dunia, kwani akiimba anajihisi kama ni binti wa miaka 14!

Mwaka 2006, Kampuni ya nchini Uingereza iitwayo Screen Station kwa kushirikiana na Busara Promotions, walitoa filamu inayoonesha hali halisi ya maisha ya Bi. Kidude, iitwayo ‘As Old As My Tongue-The Myth and Life of Bi.Kidude’.

Filamu hiyo ilikuwa ikielezea historia nzima ya maisha yake Bi. Kidude.
Fatuma Binti Baraka alikuwa anakunywa sana pombe na kuvuta sigara katika jamii isiyopenda mabadikilo lakini aliweza kuishi.

Sauti ya Bi,. Kidude alikuwa ya juu, alikuwa ni mahiri wa kuimba bila kutumia kipaza sauti.

Taarabu ni nini:

Taarab ni mchanganyiko wa muziki wa Kiarabu na Kiafrika, Taarabu ni sehemu ya mchanganyiko wa muziki wa Kiswahili na wenye kuchanganyika na Kihindi na Kiarabu, inatumia ala za udi, fidla, filimbi na ngoma.

Kwa kiasi kikubwa muingiliano wa tamaduni za Kiswahili na Kiarabu unatokana Zanzibar kuwa mji wa uliokuwa chini ya Mamlaka ya Sultan wa Oman.

Zanzibar ilikuwa kituo cha biashara ya utumwa kwa mataifa ya rasi ya Kiarabu.Mwaka 1920, Bi Kidude alikuwa akiimba rasmi katika matamasha ya kitamadauni.Bibi huyo alionesha mfano kwa wanawake hasusan wanaovaa Baibui, vazi la kujisitiri kwa wanawake wa Pwani ya Afrika Mashariki.

Bi. Kidude alionesha ujasiri mkubwa wakati alipotoroka katika visiwa vya Zanzibar kukwepa ndoa ya lazima akiwa na umri wa miaka 13.

Baadaye akawa mtu anaejihusisha sana na muziki wa taarab kwa kufanya ziara mbalimbali za muziki huo katika maeneo ya Afrika ashariki.

Baada ya kurejea Zanzibar 1940, pamoja na kuwa mtu mwenye umaarufu mkubwa lakini aliendelea kuishi katika nyumba yake iliyotengenezwa kwa udongo. Mbali na muziki alikuwa akijihusisha na 

vyama vya kijamii na kutoa elimu ya unyago kwa wasichana katika visiwa hivyo.

Taarabu ni maisha yake.

Kwa kutumia muziki wenye hisia na huzuni, Bi Kidude alikuwa akiimba kwa mtindo wa aina yake wenye mvuto.

Hakuweza kujali kuhusu miiko, aliolewa mara mbili japokuwa hakubahatika kupata mtoto.Wakati akiwa katika jukwaa alikuwa akipenda kubadili miondoko wakati wowote.

Kitendo hicho kilikuwa kikiwapa wakati mgumu sana wanamuziki wanaompiga vyombo mbalimbali katika bendi husika kwa wakati huo.

Washabiki wake walikuwa wakipenda sana mawazo yake ya kubadili miondoko au nyimbo akiwa katika jukwaa.Ingawa mwanamke huyo alikuwa mwenye umbo dogo lakini alikuwa akipiga ngoma katika kiwango cha kushangaza wengi.

Bi. Kidude alikuwa kikongwe, lakini alikuwa maarufu na mwenye kufurahisha watu wa umri tofauti hadi vijana kwa kuimba na kupiga ngoma kwa wakati mmoja.

Kila mara alikuwa akipinga kwa nguvu zote mitindo ya taarabu inayopigwa miaka hii ya karibuni, akitamka kwa kusema siyo taarab.

Bi. Kidude alikuwa akisisitiza kuwa taarab halisi wanamuziki wote huketi kwenye viti vyao, mwimbaji muongozaji ndiye aliyekuwa akisimama akishika kipaza sauti.

“toka linii taarab ikachezwa na steji shoo, kutamka matusi, kukata viuno hadharani” alilama Bi.Kidude. 

Taarab ya miaka hii imeboreshwa kutokana na wakati, siku hizi wanaita ‘Tara dance’

Mwenyezi Mungu akupe kauli thabiti, na kaburi lako liwe ni nuru miongoni mwa nuru za peponi Amina.



Makala hii imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa mitandao mbalimbali.

Mwadaaji anapatikana kwa namba: 0713331200, 0784331200, 0736331200 na 0767331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...