Na Novatus Makunga,Simanjiro,Agosti 04,2019

Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara imekabidhiwa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya shule ya msingi Loswaki iliyopo katika kata ya Terrat.

Miundombinu hiyo iliyojengwa na mingine kukarabatiwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la ECLAT Development Foundation kwa ufadhili wa shirika la Upendo Society la Ujerumani kwa gharama ya shilingi milioni 330.

Akipokea mradi huo,mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mhandisi Zephania Chaula aliwataka viongozi wa kimila la jamii ya kabila la Wamasai wanaofahamika kama Malaigwanani katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wametakiwa kutimiza kiapo chao kinachofahamika kama azimio la Namalulu kwa kuhakikisha kila mtoto wa kike anafikia elimu ya chuo kikuu.

Mhandisi Chaula aliwakumbusha Malaigwanani kutekeleza azimio lao la Namalulu ambapo alisema kuwa walikubaliana kuhakikisha kila mtoto wa kike anasoma hadi Chuo Kikuu.

Aidha Mhandisi Chaula alitoa ahadi ya kupeleka walimu katika shule hiyo mara tu wilaya hiyo itakapopokea walimu wapya.Alisema kuwa wilaya hiyo ina uhaba mkubwa wa walimu wapatao 460.

Aidha Chaula aliagiza kila shule wilayani humo kuandaa kambi za kitaalumu ambapo alisema zimeonyesha kuwa na mafanikio makubwa akitolea mfano wa shule ya Msingi Naisinyai ambayo ilikuwa inaburuta mkia lakini kwa sasa inafanya vizuri kutokana na makambi hayo.

Mhandisi Chaula pia aliwataka wazazi kuweka mpango wa kuwapatia chakula Watoto katika shule zote katika wilaya hiyo kwani alieleza kuwa wengi wao utembelea umbali mrefu hadi shule na hivyo upoteza usikivu darasani masomo kutokana na njaa.

Awali Mwenyekiti wa shirika la Upendo Dk.Fred Heimbach alimtaka mkuu wa wilaya ya Simanjiro kuhakikisha shule hiyo inapata walimu wanaohitajika ili wanafunzi waweze kupata elimu bora.Alisema kwa upande wao wamesaidia uboreshaji wa miundombinu lakini hawana uwezo wa kuchukuwa walimu kutoka Ujerumani na kuwapeleka Loswaki na hivyo akamtaka Mkuu wa wilaya Chaula kulingalia tatizo hili la walimu wa uzito mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya watoto wa Simanjiro.

Mwenyekiti wa ECLAT,Peter Kiroya Toima aliitaka jamii ya wafugaji wa Kimasai kutambua kwamba wakiendelea na mila zao bila kuzichuja wataachwa nyumba kimaendeleo na kuwataka kuhakikisha kila mtoto anahitimu baada ya kuanza shule.

“Tutaweza kutatua changamoto nyingi zinazotukabili endapo tu tutazingatia elimu kwa watoto wetu kwani mila ambazo tumekuwa tukizikumbatia kwa miaka mingi hazijatupeleka popote pale hivyo tuwe makini,”alisema.

Alisema kuwa shirika lake lenye makao makuu yake wilayani Simanjiro tangu lianzishwe mwaka 2008 limeshatekeleza miradi yenye thamani ya zaidi ya shiriki bilioni tano katika sekta ya elimu,maji,afya na maendeleo ya wanawake katika mikoa ya Manyara,Arusha na Mtwara

Naye diwani wa Terrat Jackson Materi alimtaka mkuu wa wilaya kuchukuwa jukumu la kuhakikisha kwamba shule inapata walimu ili iweze kufanya vizuri na kujinasua kutoka miongoni mwa shule kumi zilizofanya vibaya katika mtihani wa kuhitimu darasa la saba kwa msimu uliopita.

Alisema kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 800 na walimu watano tu ili iweze kufanya vizuri inahitaji walimu zaidi ya 15.Akitoa taarifa ya uboreshaji wa miundombinu ya shule hiyo,Msimamizi wa miradi wa ECLAT,Bakiri Msham alisema ulihusisha ujenzi wa nyumba 4 za walimu,madarasa 3,ofisi 2,vyoo vya matundo 32 pamoja na ukarabati wa madarasa 7,ofisi 2 na kutoa madawati 46.
 Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mhandisi Zephania Chaula(kushoto) akifungua mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya shule ya msingi Loswaki, wa kwanza kushoto aliyevaa mgolole ni mwenyekiti wa ECLAT Peter KIroya Toima
 Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Loswaki wakishuhudia makabidhiano ya mradi wa uboreshaji wa shule ya Msingi Loswaki. 
 Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Loswaki wakishuhudia makabidhiano ya mradi wa uboreshaji wa shule ya Msingi Loswaki. 
 Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula(katikati) akipokea hati za makabidhiano ya  mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya shule ya msingi ya Loswaki kutoka kwa mwenyekiti wa ECLAT Peter Kiroya Toima(kushoto) na mwenyekiti wa Upendo Dkt.Fred Heimbach(kulia)
 Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula(kushoto) akimkabidhi cheti cha shukrani kwa uboreshaji wa miundombinu ya shule ya msingi ya Loswaki mwenyekiti wa Upendo Dkt.Fred Heimbach(kulia).
 Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula(kushoto) akimkabidhi cheti cha shukrani kwa uboreshaji wa miundombinu ya shule ya msingi Loswaki mwenyekiti wa ECLAT Peter Kiroya Toima(kulia).
 Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mhandisi Zephania Chaula akimkabidhi rasmi hati ya mradi wa shule ya msingi Loswaki kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Mwalimu Ayub Mshana(katikati),anayeshuhudia katikati ni mwenyekiti wa Upendo Dkt.Fred Heimbach.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula(kushoto),mwenyekiti wa Upendo Dkt.Fred Heimbach(kulia) na mwenyekiti wa EcLAT Peter Kiroya Toima wakitoa zawadi za vifaa vya masomo kwa baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Loswaki.
Picha zote na Novatus Makunga

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...