Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk. Dorothy Gwajima akicheza mziki na walengwa wa TASAF kutoka vijiji vitano vya Kata ya Kiparang’anda wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani aliowatembelea kuona changamoto na mafanikio yao katika mpango huo.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk. Dorothy Gwajima akiandika baadhi ya kero za walengwa wa TASAF alipokutana nao kwenye kijiji cha Kiparang’anda B Kata ya Kiparang’anda wilayani Mkuranga Pwani, jana.

………………


NA MWANDISHI WETU, MKURANGA

SERIKALI imesema haitasita kuwang’oa kwenye nafasi zao Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Idara na Wataalam wa watakaoshindwa kuubeba Mpango wa Kunusuru Kaya maskini zaidi (TASAF), kwenye ajenda za vikao kazi vyao.

Hayo yalisemwa wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani jana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk. Dorothy Gwajima wakati wa kikao kazi kati yake, mkuu wa wilaya, mkurugenzi na wakuu wa idara za wilaya ya Mkuranga.


Alisema hivi sasa Serikali ipo kwenye mkakati wa kuiboresha na kuitekeleza TASAF mpya hivyo ni lazima kila idara ihakikishe walengwa wa mpango huo wanafuatiliwa kuanzia kwenye afya na shughuli zao za kiuchumi.


“Walengwa hawa wanaitwa maskini kwa sababu ya uchumi lakini wanazo nguvu na akili za kufanyakazi… ndio maana serikali imeleta TASAF kuwapa ‘starter’ wakipata chakula waende wakafanye shughuli za kiuchumi kwenye eneo lao.

“Taifa linaelekea kwenye uchumi wa viwanda hatuwezi kufika ikiwa kuna watu wanasubiri kupewa tu, hapa tunawajengea na uwezo pia kiuchumi.

“Nasisitiza kwamba lazima vikao 12 vya CMT viwe na ajenda 12 za TASAF na hili nitalisimamia kwa hakika nitapita kwenye halmashauri zote 184 za nchi hii. Nitakayekutana nae anaibagua TASAF huyo atakuwa hatoshi na inshaallah nchi hii ina watu wenye uwezo tutamtoa tutamuweka anayeuelewa mpango huu,” alisema Dk. Dorothy.

Alisisitiza kwamba TASAF ni mgoma inayotakiwa kuchezwa na wote kuanzia kitongoji hadi taifa huku maofisa ustawi wa jamii, afya, elimu, kilimo, mifugo, sheria na uchumi wakiwa sehemu ya utekelezaji wa mpango huu.

“Kwenye hili sitakubali kuona mnamuangusha Rais John Magufuli nitalisimamia hili na mazuri yote ya TASAF yaonekane… wanasema maji madogo ndio yanayozamisha watu usilidharau hili litakuzamisha,” alisisitiza Dk. Gwajima ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya TASAF taifa.

Akizungumzia Ushiriki wa Halmashauri ya Mkuranga, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Mhandisi Mshana Munde alisema baada ya kupewa elimu sahihi kuhusu TASAF amelazimika kutengeneza sheria ndogo ili Mratibu wa TASAF aingie kwenye vikao vya utendaji kila mwezi.

“Tumekuelewa na sisi kwenye vikao vyetu tumerekebisha sheria ili Mratibu wa TASAF aingie na tunapokea taarifa yake inakuwa rasmi kwenye taarifa za halmashauri, awali jambo hili halikuwepo,” alisema Munde.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...