DHAMANA ya aliyekuwa rais wa klabu ya Simba Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu, imebakia kwenye sintofahamu kufuatia mabishano makali ya kisheria baina ya upande wa serikali na ule wa utetezi, na kusababisha washitakiwa hao kurudi rumande hadi Septemba 27, mwaka huu.

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa kusudio la kukata rufaa walilopeleka Mahakama Kuu linaifanya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutoendelea na hatua yoyote ikiwemo washtakiwa hao kupatiwa dhamana hadi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Akiwasilisha hoja za upande wa mashtaka, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa wamepeleka kusudio la kukata rufaa dhidi ya uamuzi uliowaona washitakiwa hao hawana kesi ya kujibu katika mashitaka ya utakatishaji fedha, chini ya kifungu 379 (1) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Amedai kutokana na kusudio hilo, wanaomba mahakama kusimama kufanya yale yote yaliyotakiwa kufanyika ikiwemo ,washitakiwa kupewa dhamana hadi rufaa hiyo itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi katika mahakama Kuu.

Amedai, walikuwa na ushahidi wa kutosha katika mashitaka ya utakatishaji fedha na kwamba suala la kuweka masharti ya dhamana limetokana na kuwaondolea mashtaka ya utakatishaji fedha ya kwamba washitakiwa hawana kesi ya kujibu kwenye mashtaka hayo.

"Pale ambapo kuna kusudio kinachofanyika ni kuacha kuendelea kusikiliza kesi hii hadi maamuzi yatakapotolewa," amedai Wankyo na kuongeza kuwa wana haki ya kukatia rufaa maamuzi yaliyotolewa kwa sababu hayo ni maamuzi ya mwisho na hivyo, suala la dhamana libaki kama lilivyo.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Utetezi, Nehemiah Nkoko ameiomba mahakama itupilie mbali maombi ya upande wa mashitaka kwa sababu lengo lao ni kuona washitakiwa hawapati dhamana katika kesi hiyo.

Amedai, mahakama imesikiliza mashtaka yote katika kesi hiyo na kufikia uamuzi wa kuwa washitakiwa wana kesi ya kujibu katika mashitaka mengine isipokuwa ya utakatishaji fedha.

"Mahakama hii inamamlaka ya kutoa dhamana kwa sababu tayari ilishataja masharti na kilichobaki ni kuangalia kama wadhamini wametimiza masharti hayo au la," amedai Nkoko.

Ameendelea kudai kuwa, wakati mahakama hiyo ilipowaona hawana kesi ya kujibu katika mashitaka hayo mawili, upande wa mashitaka waliulizwa kama walikuwa na pingamizi wakajibu kuwa hawana pingamizi la washitakiwa kupata dhamana.

Alidai mahakama haiwezi kusimamisha utoaji wa dhamana kwa sababu tayari ilishatoa masharti.Baada ya mabishano makali ya kisheria, Hakimu Simba amesema atatoa uamuzi Septemba 27,2029 washtakiwa yao wamerudishwa rumande

Septemba 19, mwaka huu baada ya mahakama kuwakuta washtakiwa hawana kesi ya kujibu katika mashtaka ya utakatishaji, Wakili wa Takukuru Leornad Swai aliulizwa kama anapingamizi lolote juu ya dhamana alidai hawana pingamizi na Hakimu Simba aliwapatia masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 30 kwa kila mmoja pamoja na kuwa na vitambulisho.

Mbali na Aveva na Kaburu, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo, Zacharia Hanspope ambaye yeye yuko nje kwa dhamana.

Katika keai hiyo, shtaka la kwanza, Aveva na Kaburu wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka ambapo wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Marekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.

Pia wanadaiwa kwa pamoja walighushi nyaraka iliyokuwa ikionesha Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.Aveva anadaiwa katika benki ya CRDB alitoa nyaraka ya uongo ikionesha Simba wanalipa mkopo wa USD 300,000

Aveva anadaiwa kuwa katika Benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 187,817 wakati akijua zimetokana na kughushi.Kaburu anadaiwa kumsaidia Aveva kujipatia fedha hizo kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na zao la kughushi. 

Aveva, Kaburu na Hans Poppe wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya USD 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli

Katika mashitaka ya nane, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo kwa Levison Kasulwa kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya USD 40,577

Aveva, Kaburu na Hanspope wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi hizo za bandia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...