Na Mwandishi Wetu, Tunduru

WAZIRI wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt Mstaafu Georg Mkuchika,amewapongeza Watumishi wa Umma hapa Nchini kwa kuwezesha mapato ya Serikali kuongezeka kutoka Shilingi Bilioni 800  mwaka 2015  hadi kufikia Trilioni 1.7 Mwezi Septemba 2019.

Kapt Mkuchika ametoa pongezi hizo jana wakati akizungumza na  watumishi  wa wilaya ya Tunduru, wakati wa ziara yake ya siku tano mkoani Ruvuma inayolenga kusikiliza kero na kuongea na watumishi wa Umma katika wilaya zote tano za mkoa huo.

Kwa mujibu wake,mafanikio hayo ya Serikali ya yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na Watumishi Halmashauri za Wilaya,Miji,Manispaa na Majiji kutokana na kusimamia vema  mapato yanayopatikana kutoka kwenye vyanzo vya mapato.

Hata hivyo Mkuchika alisema, pamoja na makusanyo  mazuri ya kodi watumishi kutojaribu  kuzitumbuiza fedha mifukoni mwao, badala yake zielekezwe katika kuwapatia wananchi huduma Bora na za msingi kama Elimu,Maji,Afya na miundombinu mbalimbali.

Alisema,  asilimia kubwa fedha zinazokusanywa zinapelekwa kwenye Serikali za Mitaa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwataka watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru kuhakikisha wana simamia vema fedha na zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Aidha alionya kuwa,Serikali inavyo vyombo vya Dola ikiwemo Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU) ambavyo kazi yake ni kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha zinazopelekwa kwenye Halmashauri na Idara nyingine za Serikali.

Akizungumzia suala la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa Umma Kapt Mkuchika alisema,zoezi hilo ni endelevu hata hivyo limekuwa na changamoto kadhaa,lakini Serikali baada ya kubaini hali hiyo ilitoa maelekezo kuwa Watumishi wote ambao walikuwa na ajira za kudumua au  mikataba ambao walikuwa kazini kabla ya tarehe 20 Mei 2004 ulipoanza kutumika waraka wa Utumishi warejeshwe kazini na walipwe  mishahara yao hadi watakapostaafu.

Alisema, katika  zoezi hilo watumishi Elfu Moja Mia Tatu Sabini(1,370) waliolegezewa masharti  ya sifa za muundo kupitia Barua ya Katibu Mkuu Utumishi wa Umma Juni 2011, hata hivyo alifafanua kuwa haukuwahusu watumishi wale wenye vyeti vya kughushi, na walioajiriwa baada ya Mwaka 2014.

Mkuchika amewataka watumishi wa Umma,kutekeleza majukumu yao  kwa kuzingatia Weledi, na kuacha  kufanya kazi kwa mazoea, na kuacha ubabaishaji tabia ambayo inakwamisha sana malengo ya Serikali ya awamu ya tano.

Pia Mkuchika amezitaja idara ya kilimo,Maji na Utawala zinaongozwa kulalamikiwa  kuhusu vitendo vya Rushwa  na kuwataka watumishi wa Idara hizo kubadilika na kujiepusha na vitendo vya Rushwa ambavyo vinachangia kuwepo kwa miradi hewa na watumishi wa chini kukosa haki zao.

Hata hivyo baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, wamelalamikia kutopandishwa vyeo mara wanaporudi kutoka vyuoni na wengine kutolipwa stahiki zao kama fedha za uhamisho na kupandishwa madaraja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...